Jumapili, 7 Januari 2018
Mhasibu wa hospitali ya rufaa Mbeya asakwa na Polisi kwa mauaji ya mkewe, mtoto
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamsaka mhasibu wa hospitali ya rufaa Mbeya, Lucas Lukule kwa tuhuma za kumuua mkewe, mtoto na shemeji yake kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Januari 7, Kaimu kamanda wa kanda hiyo, Benedict Katalika aliwataja kwa majina waliouawa kuwa ni Upendo Lukule ambaye ni mke wa mhasibu huyo, Mageth Samwel ambaye ni shemeji yake.
Amesema tukio hilo lilitokea usiku wa Januari 4 mwaka huu nyumbani kwake eneo la Goba Matosa, jijini Dar es Salaam.
Amesema Lukule alichukua uamuzi huo baada ya kumtuhumu kwa muda mrefu mkewe kuwa mtoto wao wa miezi minne siyo damu yake, kwamba ana uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine.
Amebainisha kuwa muuaji alifanya kitendo hicho kwa kutumia jembe lililokutwa katika eneo la tukio, kisha kutokomea kusikojulikana.
Amesema walipata taarifa kutoka kwa majirani ambao walipiga simu polisi na walipofika eneo la tukio walivunja mlango wa nyumba hiyo na kukuta maiti tatu zikiwa zimetapaka damu.
“Tulipoingia ndani tulikuta jembe likiwa na damu nyingi na kukuta ujumbe ulioandikwa na muuaji ukisema Polisi tusihangaike kwa kuwa yeye ndiye aliyefanya mauaji hayo,” amesema Kitalika.
Kitalika amesema muuaji huyo ametokomea kusikojulikana hivyo jeshi la polisi linaendelea kumtafuata ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni