Jumapili, 7 Januari 2018
Hali ya kiafya ya Kingunge yaendelea kuimarika
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imesema hali ya mwanasiasa mkongwe nchini Kingunge Ngombale Mwiru, inaendelea kuimarika licha ya kuwa bado yupo katika chumba cha uangalizi maalum (ICU).
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Januari 7, Ofisa Uhusiano wa MNH, Neema Mwangomo amesema anaendelea kupatiwa huduma kwa ukaribu zaidi na jopo la madaktari.
Kingunge aliyelazwa katika wodi ya Mwaisela, alifiwa na mke wake Pares Mwiru, Alhamisi iliyopita saa nane mchana katika wodi ya Sewahaji alikokuwa amelazwa.
Mwanasiasa huyo mkongwe alifikishwa hospitalini hapo baada ya kushambuliwa na mbwa nyumbani kwake Kijitonyama, alifanyiwa upasuaji Januari 4.
“Amewekwa pale kwa ajili ya uangalizi wa karibu, ICU zina nesi katika kila kitanda lakini pia jopo la madaktari hivyo inakuwa rahisi kuifikia wodi hiyo mara kwa mara. Kwa sasa anaongea vizuri ikilinganishwa na siku mbili za nyuma,” amesema Mwangomo.
Mtoto wa Kingunge, Kinje Mwiru amesema jana walimpa taarifa kuhusu kifo cha mama yao.
“Ilikuwa ni vigumu sana wakati tunamfikishia taarifa hizo na amezipokea kwa ugumu sana. Haikuwa rahisi kwa yeye kupokea taarifa wakati tunamweleza, tumemuacha na huenda leo akatupatia mwongozo kuhusu mazishi,” amesema Kinje.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni