Alhamisi, 26 Oktoba 2017

Kichuya awatahadharisha Yanga

Mchezaji wa Simba SC, Shiza Kichuya amefunguka na kuwataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi siku ya Jumamosi ambapo Simba na Yanga watakuwa wakicheza katika uwanja wa Uhuru na kusema wao wanataka pointi tatu hivyo Yanga lazima waumie.

Shiza Kichuya amesema hayo kupitia mtandao wa kijamii wa klabu ya Simba na kusema kuwa mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi bali wanapaswa kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuwapa amasa wakati wakikipiga na klabu ya Yanga.

"Napenda kuwaahidi mashabiki na wapenzi wa Simba wajitokeze kwa wingi kuja kuipa nguvu timu yao, sisi kama timu tumejiandaa vizuri na mchezo wa Jumamosi ambao kwetu sisi ni muhimu kupata pointi tatu, napenda kuwaambia wapenzi, mashabiki wa Simba watarajie vitu vikubwa kutoka kwenye timu yao ambayo wanaimani nayo hakika tutawapa matokeo katika mechi ya Jumamosi hatutawaangusha muhimu ni pointi tatu kwetu" alisisitiza Kichuya.

Shiza Kichuya kwa mechi mbili mfululizo ambazo wamekutana watani hao wa jadi amekuwa mwiba mkali kwa Yanga kwa kuweza kuharibu mipango ya klabu hiyo ambapo katika mechi ya kwanza alisawazisha bao la Tabwe dakika za mwisho za mchezo na katika mechi ya pili aliifungia Simba bao la ushindi dhidi ya Yanga. 


Hakuna maoni: