Jumatatu, 25 Septemba 2017

CONTE ATAMANI KURUDI ITALY


Faridi Miraji , Dar es salaam.                           


Kocha wa Chelsea Antonio Conte ameweka wazi nia yake ya kurejea Italia hapo baadae baada ya kusema kwamba hana mpango wa kukaa nje ya nchi ya Italia kwa muda mrefu .

Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Italia alizawadiwa mkataba mpya wa miaka miwili majira haya ya kiangazi baada ya kuiongoza Chelsea kwenye ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza katika msimu wake wa kwanza, licha ya kwamba mkataba huo mpya haujarefusha muda wake wa kubaki darajani bali ni kuboresha kipato chake.

Lakini leo Jumatatu ameiambia radio ya Anch'io Sport," Nimepakumbuka sana Italia, hakuna shaka kuhusu hilo."

"Haipo akilini mwangu kukaa nje ya Italia kwa muda mrefu . Italia ndio nchi yangu, nitarejea, sijui ni lini lakini hilo ndio lengo langu."

Alipoulizwa zaidi kuhusu mustakabali wake wa baadae na baadhi ya nchini nyingine ambazo angependa kufanya kazi kama China na Ujerumani , Conte alijibu," China ? Hapana, hapana kabisa. Ujerumani ? Mara zote ni ngumu kutabiri maisha ya baadae. Labda tuseme kazi ya kocha ni kazi ya muda tu."

"Inategemea na matokeo , lakini kuna matamanio makubwa kwangu kufanya kazi kwa kadri ya uwezo wangu , kumaliza mradi mmoja na kutafuta mradi mwingine sahihi , nimepakumbuka sana Italia, huo ni ukweli."

"Na baadae pia ningependa kubadilisha kazi ,pengine niwe mkurugenzi wa michezo."


Hakuna maoni: