Jumamosi, 6 Januari 2018

WAUZA NYAMA WAANZISHA MGOMO


WANANCHI wilayani Nyamagana jijini Mwanza wamekosa huduma ya nyama kwa siku mbili, kutokana na mgomo wa wachinjaji walioamua kufunga maduka wakidai kupandishiwa ushuru.

Wanadai kupandishiwa ushuru wa huduma ya uchinjaji na Halmashauri ya Jiji kutoka Sh. 2,000 hadi 6,500.

Baadhi ya wananchi hususani mamalishe ambao wameathirika kibiashara, walidai kukosekana kwa nyama mabuchani kumechangia biashara zao kudorora kwa kipindi.

“Kiukweli hali ya biashara imekuwa ngumu kutokana na watu wengi tunaowauzia chakula ni wapenzi wa nyama, lakini leo (jana) ni siku ya pili mabucha yamefungwa kutokana na madai ya kupandishwa kwa ushuru, jambo ambalo linaathiri watu wengi wasio na hatia, hivyo wahusika wanahitaji kukaa na wafanyabiashara hiyo na kukubaliana na sio kuwapo kwa maamuzi ya upande mmoja,” alisema Zawadi Kitwima, mamalishe.

Mwenyekiti  wa wafanyabishara ya ng’ombe na myama Jiji la Mwanza, Makoye Lutema, alisema hawakubaliani na upandishwaji wa tozo ya gharama za uchinjaji kutokana na Mkurugenzi wa Jiji ambaye amekiuka maelekezo ya Rais John Magufuri ya kutaka kushirikisha wadau waliopo katika maeneo husika endapo mabadiliko yoyote yatatokea.

“Kukosekana kwa nyama ndani ya Jiji la Mwanza au katika halmashauri hizi mbili ni kutokana na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza kushindwa kuwa na mahusiano mazuri na wadau na kutumia mamlaka yake vibaya, cha kushangaza anapandisha tozo ya shiringi 6,500 katika machinjia ya muda ambayo haina choo wala miundombinu iliyo rafiki kwa binadamu, ni afadhari upandishwaji huu angeufanya katika machinjio mpya inayojengwa tungemuelewa na sio hii,” alisema Lutema.

Naye Mkurugenzi wa Jiji hilo, Kiomoni Kibamba, alisema hajakataa kukaa na wadau hao na kinachomshangaza, wadau hao wanamtaka aende wilayani Misungwi katika halmashauri nyingine ambayo yeye kisheria sio muhusika, huku akisema sheria hiyo ya upandishwaji wa tozo ilipangwa na vikao mwaka 2015.



Hakuna maoni: