Jumamosi, 20 Januari 2018

Washirika wa Mugabe watimuliwa bungeni

Baada ya Rais Robert Mugabe kuondolewa madarakani mwishoni mwa mwaka jana, sasa rungu hilo limeamia kwa wabunge wa Chama tawala cha ZANU-PF baada ya taarifa za kufukuzwa kwa wabunge 11 wa chama hicho kusomwa bungeni.

Wabunge hao 11 ambao wamefukuzwa wanatajwa kuwa washirika wakubwa wa Rais Mugabe.

Maamuzi ya kuvuliwa uanachama wabunge hao yalitolewa na kutangazwa Bungeni na Naibu Spika wa Bunge la Zimbabwe, Mabel Chinomona baada ya Bunge hilo kupokea barau kutoka kwenye chama cha ZANU PF iliyosema wabunge hao wamefukuzwa kwa mujibu wa Katiba ya Zimbabwe kupitia kifungu namba 129 (1) (k).

Naibu Spika alisema kuwa wabunge waliofukuzwa ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya ndani, aliyekuwa Waziri wa Nishati, aliyekuwa Waziri wa Michezo, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na wabunge wengine wa majimbo mbalimbali nchini humo.

Kufuatia zoezi hilo Bunge limetangaza nafasi zilizo wazi katika majimbo hayo 11 na kuijulisha Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe kuhusu uwepo wa nafasi za wazi katika majimbo hayo kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo ili zoezi la uchaguzi liweze kufanyika kupata wawakilishi wa Wanachi.

Hakuna maoni: