Jumamosi, 13 Januari 2018

Polisi watawanya Wakristo wakiomboleza DR Congo

Waumini wa Kanisa Katoliki waliojikusanya Ijumaa kuomboleza vifo vya watu saba waliouawa wiki mbili zilizopita katika maandamano ya kumpinga Rais Joseph Kabila walishindwa kufanya hivyo baada ya polisi kuwatawanya kwa gesi ya kutoa machozi.

Viongozi mashuhuri wa upinzani wakiwemo Felix Tshisekedi na Vital Kamerhe pamoja na wanadiplomasia walikuwepo.

Mpigapicha wa shirika la Reuters aliyekuwa akipiga picha za misa ya kuwaombea marehemu anasema polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi kutoka nje, bila shaka kuzuia mkusanyiko huo kuchukua sura ya maandamano ya kisiasa.

“Sielewi kwa nini walitufyatulia gesi ya kutoa machozi. Ukweli, serikali hii lazima iondoke,” alisema mwombolezaji mmoja wakati akikimbia wingu la gesi ya kutoa machozi lililokuwa limetanda angani na ambaye alijitambulisha kwa jina moja tu la Florence.

Watu kadhaa wameuawa katika maandamano ya kumpinga Kabila katika miaka miwili iliyopita na vurugu kutokana na wanamgambo zimeivuruga Congo na kusababisha hofu kwamba taifa hilo kubwa la Afrika ya Kati linaweza kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Umoja wa Mataifa umesema vikosi vya usalama vya DR Congo vimeua kwa uchache watu saba katika jiji la Kinshasa wakati wa mkesha wa Mwaka Mpya katika maandamano yaliyoandaliwa na wanaharakati wa Kikatoliki kupinga hatua ya Kabila kukataa kuachia madaraka.

Mkuu wa Kanisa Katoliki DR Congo, Pierrot Mwanamputu, siku mbili baadaye alilaani kuwa ukandamizaji “hauna zaidi wala hauna pungufu ya unyama”.

Polisi, ambao wanakiri kuua watu wanne tu, wanadai waliouawa walikuwa wapiganaji na wahalifu.

Hakuna maoni: