Jumamosi, 20 Januari 2018

Museven asema malezi ya Kikristo yalimzuia kunyonga

Rais Yoweri Museveni amesema upo uwezekano wa sheria ya kunyonga kurejeshwa ikiwa ni miaka 13 tangu aliponyongwa mtu wa mwisho.

Museveni amesema "malezi ya Kikristo" yalimzuia kuendeleza adhabu ya kifo lakini sasa anaona “huruma” inachochea ongezeko la wahalifu.

Katika Uganda, kuna makossa 28 ambayo adhabu yake ni kunyongwa kwa waliokutwa na hatia, idadi ambayo ni kubwa kwa nchi za Afrika Mashariki. Ripoti zinaonyesha watu 278 wanasubiri kunyongwa.

"Nimekuwa naacha kuridhia kunyongwa kwa waliopatikana na hatia kwa sababu ya malezi yangu ya Kikristo lakini huruma imekuwa ikisababisha watu kufikiri wanaweza kudhuru wengine na wasifanywe lolote," amesema Museveni katika ujumbe wa Twitter.

Vilevile alisema “atanyonga wachache” wakati wa sherehe za kuhitimu wahudumu wa magereza jijini Kamapala.

Hata hivyo makundi ya watetezi wa haki za binadamu wameonya dhidi ya hatua hiyo kutokana na udhaifu mkubwa katika upelelezi. "Kunyonga wafungwa hakuwezi kumaliza uhalifu," mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya haki za binadamu ya FHRI, Livingstone Ssewanyana aliliambia shirika la Washington Post.

"Polisi ni wadhaifu mno na hawana uwezo wa kufanya uchunguzi makosa kwa kina. Matokeo yake mfumo mzima haufanyi kazi."

Katika miaka ya hivi karibuni uhalifu umeongezeka huku wanawake 20 wakiuawa katika miezi minne tu katika jiji la Kampala mwaka jana. Baadhi ya wakosoaji wanasema polisi wameweka juhudi kubwa dhidi ya wakosoaji wa Rais Museveni kuliko kukamata wahalifu.



Hakuna maoni: