Jumanne, 9 Januari 2018

Msekwa afunguka kuhusu wanaohama vyama


Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM Bara, Pius Msekwa amesema hamahama ya wabunge na madiwani inayosababisha nchi kuingia katika chaguzi ndogo kuziba nafasi zilizoachwa wazi ni tatizo ambalo wakongwe katika siasa, akiwamo yeye waliliona miaka mingi iliyopita.

Amesema akiwa Spika wa Bunge kuanzia Aprili 1994 hadi Desemba 2005, chombo hicho cha dola kiliona tatizo hilo na kupitisha sheria ya kuruhusu chaguzi ndogo kufanyika mara moja ndani ya miaka mitano, lakini ilifutwa na Mahakama kabla ya kuanza kutumika.

“…Tuliokuwepo katika madaraka kwa muda mrefu tuliwahi kuliona hili kwamba uchaguzi mdogo unaigharimu Serikali na walipa kodi pesa nyingi. Kwa hiyo nikiwa Spika wa Bunge tukapitisha sheria kwamba tusifanye uchaguzi mdogo kila unapotokea, tufanye uchaguzi mdogo mara moja katika miaka mitano,” alisema Msekwa.

Mbunge huyo wa zamani wa Ukerewe alitoa kauli hiyo jana baada ya kuulizwa na Mwananchi nini mtazamo wake kuhusu wanasiasa, hasa wabunge na wadiwani wanaohama vyama vyao na kusababisha chaguzi za mara kwa mara kuziba nafasi zao.

Alisema licha ya wanaohama kuwa na haki ya kufanya hivyo, chaguzi za marudio zinatumia fedha nyingi ambazo ni kodi ya wananchi.

Alibainisha kuwa sheria hiyo ilifutwa baada ya wanaharakati kufungua kesi mahakamani na chombo hicho cha kutafsiri sheria kueleza kuwa hatua hiyo ingewanyima haki wananchi kuwa na wawakilishi bungeni.

Katika kipindi cha mwaka mmoja kumekuwa na wimbi kubwa la wabunge na madiwani kuvihama vyama vyao, huku madiwani sita wa Chadema katika jimbo la Arumeru waliojiunga na CCM wakifungua dimba. Mpaka sasa Chadema kimepoteza madiwani zaidi ya 17 na mbunge mmoja ambao wote wamehamia CCM.

Aliyekuwa mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia naye alihamia CCM huku aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu akihamia Chadema.

Desemba 31 mwaka jana wakati akihojiwa na kituo cha Televisheni cha Azam, Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aligusia hamahama hiyo akisema haina tija kwa Taifa na ni aibu kwa vyama vyote, ikiwamo CCM.

Alisema suala hilo likiachwa liendelee litazua migogoro na hakuna chama kitakachobaki salama kwa kuwa linapuuza juhudi za wanachama waliokulia ndani ya chama na kutukuza wapya.

Katika ufafanuzi wake kuhusu sheria hiyo iliyofutwa Msekwa alisema, “Kwamba ikitokea mbunge amekufa, amehama au kwa sababu yoyote nafasi ikabaki wazi basi inaachwa wazi mpaka katikati ya kipindi (cha miaka mitano) ndio unafanywa uchaguzi mdogo kwa kujaza nafasi zote kwa pamoja.

“Halafu baada ya hapo mnasubiri uchaguzi mkuu unaofuata. Tulidhani hiyo itapunguza gharama za mara kwa mara na Tume ya Uchaguzi (NEC) itengeneze bajeti yake kwa kujua kuwa uchaguzi uko mbali.”

Alisema sheria hiyo ililenga majimbo au kata zinapoachwa wazi, uchaguzi wa kuziba nafasi hizo ufanyike kwa pamoja baada miaka miwili na nusu baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.

“Tulifikiri hiyo itasaidia kupunguza kimbiakimbia ya uchaguzi na kampeni kama inavyofanyika sasa,” alisema na kuongeza,

Awali, akizungumzia uhuru wa mtu kuhama chama kimoja na kwenda kingine alisema, “Sioni kwa nini watu linawashangaza. Tafsiri yake ni watu kuwa na uhuru wa kujiunga na chama alichokitaka. Usimbane mtu mpe uhuru huo.”

“Kila mtu ana uhuru wa kubadili vyama ndio maana watu wanatoka CCM kwenda upinzani na kutoka upinzani kwenda CCM.”

Hakuna maoni: