Rais John Magufuli ameamua kuweka bayana udhaifu wa mawaziri wa madini na kilimo, manaibu na watendaji wao, akiwapa wiki moja, huku akiweka bayana kuwa kuna baadhi ya wateule wake bado hawajamuelewa anataka nini.
Rais pia ametengua kwa mara ya kwanza mwaka huu uteuzi wa Kamishna wa Madini, Benjamin Mchwampaka, ambaye aliteuliwa Aprili mwaka jana, kwa kushindwa kumshauri Waziri wa Madini kuhusu kanuni za Sheria ya Madini Namba 7 ya mwaka 2017.
Rais alitoa yake ya moyoni jana wakati wa hafla ya kumuapisha Dotto Biteko kuwa naibu waziri wa Wizara ya Madini, akisema “labda ataenda kuamsha waliolala” kwenye wizara hiyo.
“Wizara ya Madini ina changamoto nyingi na hata sasa hivi bado ina changamoto nyingi,” alisema Rais ambaye alianza kwa sauti ya chini hotuba yake katika hafla hiyo iliyorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Serikali, TBC1.
“Na niseme tu, ukiachia mambo machache machache, bado Wizara ya Madini haifanyi kazi vizuri sana. Unajua nikizungumza kwa kupamba nitakuwa mnafiki.”
Rais alizungumzia jinsi Sheria ya Madini ilivyopitishwa na jinsi itakavyofanya kazi ya kuinufaisha nchi na ndio maana ilipofika mezani kwake aliisaini bila ya kuchelewa na kuagiza watendaji wake washughulikie kanuni.
“Sasa kuanzia mwezi wa saba baada ya kupitisha Sheria Namba 7 ya mwaka 17, mpaka leo regulations (kanuni) hazijasainiwa. Waziri yupo; naibu waziri yupo; kamishna ambaye ndio mshauri mkuu wa waziri yupo; wakurugenzi wapo,” alisema Rais.
Angella Kairuki, ambaye kwa sasa yuko likizo, ndiye Waziri wa Madini baada ya Rais Magufuli kuitenga wizara hiyo na Nishati. Naibu wake ni Stanslaus Nyongo, ambaye alisifiwa kwa kufanya ziara migodini, wakati hadi jana kamishna alikuwa Mchwampaka.
Alisema watendaji wizara hiyo bado hawajakata kiu yake katika utendaji.
“Unaweza kujiuliza kwamba tuna matatizo (gani) makubwa sisi Serikali. Kwa sababu kama zile regulations hazijasainiwa, unategemea nini?” Alihoji.
“Kwa hiyo kuanzia mwezi wa saba hawakusaini, mwezi wa nane, wa tisa, wa kumi, wa kumi na moja, wa kumi na mbili. Leo tuko mwezi wa kwanza. Miezi saba, lakini sheria imepitishwa na Bunge.”
Rais hakusita kueleza hisia zake kuhusu utendaji huo.
“Nasema hii kwa uchungu mkubwa kwa sababu baadhi ya ninaowateua bado hawajanielewa na inawezekana bado hawajaelewa Bunge linataka nini, Watanzania wanataka nini,” alisema.
“Na ndio maana nikaona labda ngoja niongeze naibu waziri aliyekuwa kwenye kamati ya madini, ili ushauri uliokuwa unatolewa na Bunge; ili haya mapendekezo yaliyopelekwa bungeni kupitia kamati yao, labda ataweza kutoa changamoto kwa watu waliolala, ambao bado wamelala ndani ya Serikali.
“Sifahamu Wizara ya Madini ina ugonjwa gani. Mtu unamteua pale, lakini sioni ile movement (shughuli) ninayoitaka and this is fact (huu ni ukweli).”
Alisema wizara hiyo ni kama ina mapepo maana kila anayepelekwa anakuwa hachukui maamuzi yaliyo sahihi.
“Ni kweli kuna hela na madhahabu haya ni kama mapepo tu. Inawezekana yanawaharibu akili halafu hamchukui maamuzi mazuri,” alisema.
Magufuli alishauri watendaji hao wamtangulize Mungu kama wanaona wanashindwa kukabiliana na matatizo ya wizara hiyo.
“Tangu sheria hii ipitishwe wizara hii haijani-impress (haijanivutia) na waziri hajani impress lakini I hope (natumanini) mtabadilika,” alisema.
Alisema kutokuwepo kwa kanuni kunaathiri hata minada na ndio maana alizuia mnada wa Tanzanite usiku mwingi ili kuepusha utapeli kwa kuwa ingeuzwa kwa thamani ndogo.
“Nikazuia usiku wa saa sita kwamba uzeni kilo zisizozidi mia tano au mia nne na kitu. Ndipo wakauza na value ikapanda juu. Wakapata Sh1.8 bilioni nafikiri na mrabaha,” alisema.
“Lakini huu si utaratibu kwa sababu sheria na regulations hazijapitishwa na ndiyo maana nikasema huu mnada hautafanyika tena mpaka hizi regulations zisainiwe,” alisema.
Rais Magufuli alisema kwa kuwa wizara imekuwa na manaibu wawili pamoja na waziri, anatumaini kanuni hizo zitasainiwa ndani ya wiki hii na kumtaka Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi kuhakikisha hilo linafanyika kabla ya Ijumaa.
Kuhusu kamishna wa madini, Rais alisema amepata taarifa kuwa mtendaji huyo ndiye kikwazo na hivyo akasema ameshamteua mtu mwingine.
“Nilikuwa naambiwa pia kamishna ni tatizo. Inawezekana yupo hapa amekuja kumpokea naibu waziri. Nimeamua kumteua mtu fulani hivi. Sijui nitalikumbuka jina, lakini jina la kwanza linaanza na Profesa Shukruni Elisha Manya. Nafikiri something like that. Ni mwalimu pale chuo kikuu, ni geologist (mtaalamu wa miamba),” alisema.
“Nililetewa mapendekezo ya watu wa palepale, nikaona ngoja nisichukue kabisa hapa. We should start with a new page (lazima tuanze na ukurasa mpya), mtu ambaye hajawa contaminated (hajachafuliwa). Kwa hiyo huyu Manya ndio atakuwa kamishna na ndiye atakuwa mtendaji mkuu wa Kamisheni ya Madini.”
Rais alisema hayo muda mfupi baada ya Biteko kueleza imani yake kwa Waziri Kairuki kuwa ni mchapakazi, akisema ana bahati kama ya Magufuli ambaye alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa naibu, alipokelewa na waziri mwanamke.
“Na mimi, Mheshimiwa Rais, umenipa heshima kubwa sana ya kuhudumu chini ya waziri mwanamke ambaye ni mchapakazi kweli,” alisema Biteko baada ya kuapishwa.
“Mimi naamini kazi yangu haitakuwa kubwa sana, itakuwa kazi ya kumsikiliza waziri wangu, kusikiliza miongozo ya Serikali na kutenda kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Niko tayari kufanya kazi kwa nguvu zangu zote kadri miongozo itakavyokuwa. Na namuomba Mungu, sala yangu na dua yangu nisijutie uteuzi wako hata siku moja.”
Waziri Kairuki, mmoja wa mawaziri wazoefu katika Baraza la Mawaziri la sasa, na naibu wake, Stanslaus Nyongo waliteuliwa Oktoba 7, 2017 katika mabadiliko yaliyotokana na kutenguliwa kwa uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Madini na Nishati, kujiuzulu kwa George Simbachawene, aliyewahi kuongoza wizara hiyo, Edwin Ngonyani ambaye alitajwa katika kashfa ya biashara ya almasi kutokana na majukumu yake wakati akiwa Shirika la Madini la Taifa (Stamico).
Muhongo alifutwa kazi kutokana na kashfa ya usafirishaji nje mchanga wa madini maarufu kwa jina la makinikia.
Kikaango cha Rais Magufuli pia kilimkumba Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba kutokana na kutosambaza vyema mbolea mikoani.
“Kwa mfano, ipo mikoa ambayo haijapelekewa mbolea, mmojawapo ni mkoa wa Rukwa na mkoa gani. Wakati tunazungumzia the big four (mikoa ya Mbeya, Rukwa, Songea na Iringa inayozalisha kwa wingi mazao ya chakula) kwa ajili ya production ya chakula, lakini mbolea hazijapelekwa,” alisema Rais.
“Lakini Waziri wa Chakula yupo na kwenye bajeti alipitisha. Nimeshatoa maagizo kwa Waziri Mkuu, mbolea zisipofika huko ndani ya wiki hii, huyo anayehusika na kupeleka mbolea aachie kazi.
“Nilishasema wale wote ninaowateua mimi wasifikiri ni sherehe, wanakuja kufanya kazi. Kwamba hawezi kufanya kazi, asikubali uteuzi wangu. Na (katika) uteuzi wangu nataka tukasolve (tukatatue) matatizo ya wananchi maskini.”
Pamoja na kumpongeza, Rais alimpa pole Biteko akisema akafanye kazi kwa sababu suala la kufukuza kwake ni la kawaida.
“Tujifunze sisi viongozi kuwa mfano mzuri kwa wananchi wetu, kazi hizi za uongozi ni mateso,” alisema Rais Magufuli.
“Ni mateso na ni msalaba mkubwa. Hizi juhudi tunazozifanya msifikirie watu wanafurahi sana, yawezekana yapo mataifa makubwa yanachukia.”
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni