Abiria wa kampuni ya ndege ya Fastjet wamekwama kusafiri kwenda Mwanza ikielezwa ndege imepata hitilafu ya kiufundi.
Wasafiri hao wamekwama leo Jumatatu Januari Mosi, 2018 saa mbili asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam. Abiria zaidi ya 30 walikwama uwanjani hapo.
Mwandishi wa MCL Digital aliwashuhudia abiria wakizunguka huku na kule kupata ufumbuzi wa safari.
Zenusta Alex aliyekuwa asafiri na ndege hiyo amesema alitoka nyumbani mapema na ndege ilitakiwa kuondoka saa nne asubuhi.
“Nilipowauliza wahusika wakanieleza kuna tatizo la hitilafu la kiufundi, nikajiuliza sasa kama ni hivyo kwa nini hawakutueleza mapema badala yake wanatuambia safiri ni hadi keshokutwa,” amesema Alex.
Amesema alikata tiketi ya Januari Mosi hadi 5 na alikuwa asafiri kuelekea Mwanza na ndugu zake saba.
Abiria mwingine, Sandra Mshomi amesema ni utaratibu mbovu uliowekwa na Fastjet kwa kuwa linapotokea tatizo kama hilo kampuni inapaswa kuhakikisha abiria wanafika sehemu husika.
Ofisa Uhusiano na Masoko wa Fastjet, Lucy Mbogoro amesema tatizo hilo la kiufundi linashughulikiwa na wataalamu. Amewaomba radhi abiria kwa niaba ya kampuni hiyo.
“Fastjet inathamini usalama, ndiyo maana mafundi walivyoona kuna hitilafu wakasema ndege haifai kuruka. Hata hivyo, mafundi wapo kazini kushughulikia changamoto hii na kesho inaweza kuruka,” amesema Lucy.
Mwananchi.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni