Alhamisi, 28 Desemba 2017

Walimu wapya waanza kuripoti Tamisemi

SERIKALI imesema baadhi ya walimu waliopo katika orodha ya walimu wapya 3,033 waliopata ajira katika shule za msingi na sekondari ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi na walimu walioondolewa kwenye utumishi wa umma baada ya kubainisha kuwa na vyeti vya kughushi, wameanza kuripoti.

Aidha imeendelea kusisitiza kuwa walimu watakaobainika kuchukua posho ya kujikimu na baadaye kuondoka kwenye vituo vyao vya kazi baada ya kuripoti watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo alisema hayo jana alipokuwa akizungumzia maendeleo ya mpango huo unaotarajiwa kukamilika ifikapo Januari 7, mwakani. Jafo alisema kuwa kati ya walimu hao, walimu 266 ni wa sekondari na walimu 2,767 ni shule za msingi.

Alisema walimu hao wanatakiwa kuripoti katika vituo vya kazi wakiwa na vyeti vya kidato cha nne na sita na vyeti vya taaluma vya kuhitimu mafunzo ya ualimu kwa ngazi husika na cheti cha kuzaliwa.

“Walimu walioajiriwa watatakiwa kuripoti katika ofisi za wakurugenzi wa halmashauri zilipo shule walizopangiwa na kisha watakwenda kuripoti kwenye shule husika. “Vituo vyao vya kazi ni shule za msingi na sekondari kwa waliopangiwa kufundisha elimu ya msingi au sekondari na si makao makuu ya halmashauri,” alisema.

Jafo aliongeza kuwa, “kila mwalimu amepangiwa kwenye shule ambayo haina walimu wa somo husika kabisa au kuna upungufu mkubwa shuleni.” Alisema waajiriwa wapya hawatahamishwa kutoka shule moja kwenda shule nyingine ndani au nje ya halmashauri au mkoa bila ridhaa ya ofisi ya Rais Tamisemi.

“Nachukuwa fursa hii kuwataka wakurugenzi katika halmashauri ambazo walimu hawa wataripoti, kuwapokea walimu hao kwa kuzingatia taratibu na kanuni za utumishi wa umma na baadaye kutoa taarifa ya kuripoti kwao,” alisema.

Hakuna maoni: