Mtoto Lucia Thomas (12), amekutwa akiwa ameuawa na mwili wake kutupwa eneo la makaburi mtaa wa mkoani mjini Geita.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkoani, Salvatory Edward amedai pamoja na kunyongwa hadi kufa, mwili wa mtoto huyo aliyehitimu darasa la saba mwaka huu katika Shule ya Msingi Kiandege wilayani Bunda pia ulikuwa na dalili za kubakwa kabla ya kuuawa.
“Mtoto huyu alikuja Geita kwa mama yake kwa ajili ya masomo ya kujiandaa na kidato cha kwanza mwakani baada ya kufaulu mitihani ya darasa la saba katika Shule ya Msingi Kiandege Wilaya ya Bunda mkoani Mara alikokuwa akisoma,” amesema Edward
Ingawa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo kwa kile alichosema ni kuepuka kuharibu uchunguzi unaoendelea, mama mzazi wa mtoto huyo, Mary Thomas amethibitisha mwili wa mwanaye kukutwa katikati ya makaburi akiwa tayari amefariki.
“Siwezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu nitaharibu upelelezi; subirini tukamilishe uchunguzi wetu,” amesema Kamanda Mwabulambo
Huku akibubujikwa machozi, mama huyo amesema mwanaye alitoka nyumbani jana Alhamisi saa 12:30 jioni akiwa ameongoza na mtu aliyesema ni mwalimu wake wa masomo ya maandalizi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa maelezo kuwa anaenda kuchukua karatasi za mitihani ya somo la Uraia.
“Mmoja wa walimu wanaomfundisha tuition alifika hapa nyumbani na kumtaka aende naye kwake (kwa mwalimu), kuchukua karatasi za mitihani ya Uraia ili aje kuyafanya usiku lakini hadi giza linaingia hakuwa amerejea,” amesema Mary
Amesema baada ya kuona usiku umeingia bila mtoto kurejea nyumbani, alikwenda kwa mwalimu mwingine aliyemtaja kwa jina moja la ambapo waliongoza hadi nyumbani kwa mwalimu aliyeondoka na mwanaye na kumkuta lakini akawatoroka kwa kujifanya anampa mtu begi alilolishika mkononi.
“Baada ya kufika na kugonga, mwalimu yule alitoka nje akiwa na begi la nguo mkononi na kutudanganya kuwa kuna mtu nje ya geti anamkabidhi begi hilo, lakini hakurejea tena,” amesema
Baada ya mwalimu huyo kutorejea huku mtoto haonekani, waliendelea kumtafuta mtoto wake usiku kucha bila mafanikio ndipo alipoenda kutoa taarifa polisi alikotakiwa kurejea iwapo itapita saa 24 bila mtoto kurejea nyumbani.
“Kabla ya saa 24 kumalizika, taarifa zilinifikia kuwa mwili wa mwanangu umeonekana makaburini akiwa tayari amefariki huku ukiwa na michubuko shingoni na akiwa amefungwa kamba miguuni huku hana nguo ya ndani,” amesema kwa uchungu mama huyo
Kutokana na tukio hilo, uongozi wa serikali ya mtaa wa mkoani umepiga marufuku vituo vyote vya masomo ya ziada eneo hilo na kuwataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kwenye shule zinazotambulika kisheria badala ya vituo vya vichochoroni.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni