Ijumaa, 10 Novemba 2017

Wafanyabiashara wahofia magonjwa ya mlipuko Mbeya

Wafanyabiashara  wa Soko la Soweto katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya wameilalamikia Halmashauri ya Jiji, kwa kushindwa kuzoa taka kwa wakati katika soko hilo, na kusababisha mlundikano mkubwa wa taka, hivyo kuhofia kupata magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu na kuhara.

Channel Ten imetembelea soko la Soweto na kujionea mlundikano wa taka, na kuzungumza na uongozi wa soko na wafanyabiashara, ambapo wameulalamikia uongozi wa jiji la Mbeya kwa kushindwa kuzoa taka kwa wakati, na kwamba wao wamekuwa wakitoa ushuru kwa wakati, lakini linapofika suala la uzoaji wa taka Halmashauri inasema haina mafuta kwaajili ya magari ya taka.

Aidha Wafanyabiashara hawa wanasema pamoja na changamoto ya taka, lakini pia walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya choo, ambapo wamelazimika kujitolea fedha na kujenga choo cha kisasa ,baada ya choo cha awali kinachomilikiwa na Jiji kuwa kwenye mazingira hatarishi kutokana na matundu kuwa machache na mazingira machafu baada ya kuwa hakifanyiwi usafi na mzabuni aliyepewa tenda ya usafi.

Choo hiki kimejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 14.2 ikiwa ni mchango wa Wafanyabiashara wa soko hili, ambapo kimefunguliwa na wafanyabiashara wenyewe bila kushirikisha uongozi wowote wa serikali , kwa madi ya kuhofia kuhusishwa na masuala ya kisiasa

Hakuna maoni: