Jumanne, 7 Novemba 2017

Upinzani wamwaga laana kisa Lissu

NAIBU WAZIRI KIVULI WA FEDHA NA MIPANGO, DAVID SILINDE.

KAMBI Ramsi ya Upinzani Bungeni imelaani bungeni kile ilichokiita jaribio la mauaji dhidi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).

Pia imelaani na kupinga kile ilichokiita vitendo viovu vya uonevu, ukandamizaji na utekaji unaofanywa dhidi ya wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani nchini.

Naibu Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, David Silinde, alilaani vitendo hivyo kwa niaba ya kambi hiyo, wakati akiwasilisha maoni kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2018/19 bungeni mjini hapa jana.

Alisema ikiwa vitendo hivyo vitaachwa viendelee bila kukemewa na kushughulikiwa kwa uzito unaostahili, kuna hatari kundi linalohisi kuonewa likakosa uvumilivu na hivyo kuathiri amani ya nchi.

Alisema ni miezi miwili sasa imepita tangu Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa kambi hiyo anusurike kifo baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi wakati wa mkutano uliopita wa bunge ukiwa unaendelea na mpaka sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na Jeshi la Polisi juu ya kukamatwa kwa watu waliohusika na tukio hilo.

"Ikiwa polisi wameshindwa kufanya uchunguzi na kuwakamata wahalifu hao ndani ya miezi miwili, Kambi Rasmi ya Upinzani haioni muujiza wowote unaoweza kutendeka ili watu hao wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria hata kama polisi wataongezwa miezi mingine miwili," alisema.

Hata hivyo, shahidi muhimu katika shambulio dhidi ya Lissu, dereva wake Simon Bakari, mpaka sasa ameshindwa kufika polisi kuwasaidia katika upelelezi huo pia.

Silinde ambaye ni Mbunge wa Momba (Chadema), alisema tafsiri ya ukimya huo wa serikali ni rahisi; kwamba hakuna dhamira ya dhati wala utayari wa kushughulikia suala hilo.

"Si nia yangu kuorodhesha matukio mabaya wanayofanyiwa viongozi wa upinzani hapa nchini kwa kuwa ni mengi na pia tumeyasema sana humu bungeni; na kwa wakati mwingine kuamriwa kuyafuta katika hotuba zetu, lakini hili la kuanza kutuwinda kwa lengo la kutuua, hatuwezi kamwe kulinyamazia," alisema.

Silinde alisema kambi hiyo inatoa wito kwa wananchi wote kupaza sauti zao kupinga uonevu na ukandamizaji wa haki, kupinga matukio ya utekaji utesaji na umwagaji damu katika nchi.

Alisema kambi hiyo pia inatoa wito kwa waumini wa dini na madhehebu mbalimbali kuendelea kumwomba Mungu awaponye wale wote walioathirika na matukio hayo lakini zaidi kuliepusha taifa na laana kwa damu ya watu wasio na hatia iliyomwagika nchini.

Silinde alisema kuwa ili Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka ujao ufikie malengo yaliyokusudiwa, ni lazima utekelezwe watanzania wakiwa na umoja na mshikamano kama taifa.

Lissu (49), ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), alishambuliwa kwa kupigwa risasi 32 na watu wasiojulikana akiwa ndani ya gari nyumbani kwake alipokuwa akitokea bungeni mjini hapa Septemba 7. Tano zilimpata.

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, mara kadhaa amekaririwa akieleza kuwa dereva wa Lissu anapaswa kujitokeza kuhojiwa na jeshi hilo akiamini ni mtu muhimu katika uchunguzi wa tukio la kushambuliwa kwa mtaalamu huyo wa sheria.

DODOMA SALAMA
Awali wakati akitoa taarifa yake bungeni jana asubuhi, Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliwahakikishia wabunge kuwa Dodoma safari hii ni salama zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Ndugai alisema:

“Nitumie fursa hii kuwakaribisha Dodoma, Dodoma ni njema, tumehakikisha safari hii Dodoma ni salama zaidi kuliko wakati mwingine wowote; msiwe na wasiwasi na Dodoma, karibuni sana."

Spika Ndugai pia alimwapisha Janeth Masaburi ambaye aliteuliwa kuwa mbunge hivi karibuni na Rais Magufuli.

Source: Nipashe

Hakuna maoni: