Jumanne, 7 Novemba 2017

Simba kuitumia City kuiua Prisons

KOCHA WA SIMBA, JOSEPH OMOG.

KOCHA wa Simba, Joseph Omog, amesema mchezo wao dhidi ya Mbeya City umewapa picha ya nini wakifanye ili kupata ushindi kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Tanzania Prisons.

Baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya mwishoni mwa wiki, Simba itashuka tena kwenye uwanja huo kucheza na Tanzania Prisons Novemba 18, mwaka huu.

Akizungumza na Nipashe kutoka mkoani Katavi walipoenda kucheza mchezo wa kirafiki ikiwa ni sehemu ya mandalizi yao, Omog, alisema wanafanya maandalizi ya mapema kukabiliana na maafande hao wa Jeshi la Magereza.

“Upinzani tulioupata dhidi ya Mbeya City naamini tunaweza kuupata dhidi ya Prisons, tayari tumeanza mikakati kuhakikisha tunashinda mchezo huo, kuja kwetu Katavi ni kwa ajili ya mazoezi kabla ya kurejea tena Mbeya,” alisema Omog.

Alisema mchezo wao wa kirafiki wa jana dhidi ya Nyundo FC ni sehemu ya mazoezi yao kujiweka sawa.

Omog alisema wachezaji ambao wameenda kuungana na kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ wataungana nao jijini Mbeya mara baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Benin.

“Mipango ni kwamba mara baada ya mchezo huo na Benin wachezaji watakuja moja kwa moja Mbeya na sisi tutakuwa tumesharejea kutoka huku Katavi,” aliongezea kusema Omog.

Mratibu wa Simba, Abbas Alli, mapema aliliambia Nipashe jana kuwa kikosi hicho kinatarajia kurejea Mbeya mara baada ya mchezo wa jana.

“Tunatarajia kurejea Mbeya kuendelea na maandalizi yetu, kama kutakuwa na mabadiliko kwa maana kama timu itaendelea kubaki huku (Katavi ) au vinginevyo tutasema ila kwa sasa ratiba ni kwamba tunarejea Mbeya,” alisema.

Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, ipo kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imefikisha pointi 19 baada ya kucheza michezo tisa sawa na Azam, lakini Wekundu wa Msimbazi hao wakiwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Hakuna maoni: