Ijumaa, 3 Novemba 2017

Taarifa ya Mkude kurudishwa Taifa Stars

Viungo wa Simba Jonas Mkude na Mudathir Yahya wa Singida United wameongezwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars.

Kocha wa timu hiyo Salum Mayanga amelazimika kuwaita viungo hao leo kwaajili ya kuziba nafasi za wachezaji Erasto Nyoni na Muzamiru Yassin ambao wana kadi nyekundu.

TFF imepata ufafanuzi wa kadi hizo ambazo walipata kwenye mchezo wa kalenda ya FIFA dhidi ya Malawi hivyo hawana haki ya kucheza mchezo ujao ambapo Stars itasafiri kuifuata Benin.

Kwa mujibu wa FIFA, Nyoni na Muzamiru wataukosa mchezo ujao dhidi ya Benin kutokana na Kanuni za Nidhamu za FIFA ambako kifungu cha 18 (4) kinaelekeza mchezaji mwenye kadi nyekundu kuukosa mchezo unaofuata.

Mkude na Mudathir watajiunga kambini na wachezaji wengine walioitwa katika kambi itakayoanza Novemba 5, mwaka huu kujiandaa na mchezo huo wa kirafiki dhidi ya Benin utakaochezwa kwenye tarehe za kalenda ya FIFA Novemba 12, huko Benin.


Hakuna maoni: