Jumatano, 8 Novemba 2017

Mbunge mwingine wa Chadema akamatwa Mtwara

Mtwara. Mbunge wa Jimbo  la Ndanda na mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini , Cecil Mwambe anashikiliwa na Jeshi la polisi Mkoani Mtwara.

Mwambe anaendelea na mahojiano juu ya tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani jana mjini Mtwara.

Mwambe aliwasili katika Ofisi  Mkuu wa  upelelezi makosa ya Jinai  Mkoa wa Mtwara   (RCO) saa 6 mchana na kutoka saa 10 na kupelekwa katika kituo cha polisi.

Akizungumza wakili wake kutoka kampuni ya uwakili ya Phoenix, Rainery Songea amesema mteja wake anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi katika mkutano wa kampeni.

"Inadaiwa katika kampeni za udiwani kuna baadhi ya maneno ambayo aliyatamka yanayosababisha  watu kufanya makosa, mwanzoni alihojiwa na askari wengine lakini kamanda wa polisi mkoa ameagiza ahojiwe na RCO  ndio tunasubiri," amesema Wakili Songea

Akizungumza mratibu wa mahusiano na mawasiliano mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni mhamasishaji,  Tambwe Hiza amesema kitendo cha ofisi ya mkuu wa upelelezi mkoa kutoa dhamana na kisha RPC kuagizwa ahojiwe upya huenda ni njama za kuvuruga kampeni zao.

"Jana walimuita aje leo asubuhi amekuja, sasa kuna tatizo gani tena leo kama ana jambo lolote na yeye wasimwambie aje kesho..ndio maana tunapata wasiwasi labda kuna njama za kuvuruga kampeni zetu za kesho (Alhamisi) wilayani Ruangwa," amesema Hiza

Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, DCP Lucas Mkondya alipotafutwa hakupatikana.

Mwananchi:

Hakuna maoni: