Jumatatu, 16 Oktoba 2017

Wagonjwa waenda na mashuka, neti hospitali

Hospitali ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mashuka, blanketi pamoja na vyandarua, hali ambayo inawalazimu wagonjwa kuchukua na kutumia mablanketi na mashuka kutoka majumbani mwao.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Kahama Dr. Fredrick Malunde amekiri kuwepo kwa changamoto hizo na nyinginezo zinazoikabili hospitali hiyo, ambapo pia amesema hospitali imeelemewa na wagonjwa wanaolazwa kwa idadi ya 30,000 kwa mwezi, huku kukiwa na wastani wa wagonjwa 200 wanaolazwa kwa siku.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kahama mji Bi. Flora Sangiwa amesema uchakavu wa miundombinu ya matibabu katika hospitali ya Kahama, unachangiwa na ufinyu wa bajeti inayotengwa lakini pia hospitali inahudumia wagonjwa wengi kutoka nje na ndani ya wilaya hiyo.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya wadau wa afya wilayani humo wamejitokeza na kuanza kutatua changamoto hiyo ambapo Benki ya Posta Tanzania tawi la Kahama wametoa mashuka 100 na vyandarua 50, huku wakidai kuendelea kutoa msaada zaidi kwa lengo la kuokoa maisha ya wagonjwa wanaolazwa katika hospitali hiyo.



Hakuna maoni: