Ijumaa, 6 Oktoba 2017

Omog ajipanga kuongeza ‘dozi’


KOCHA MKUU WA SIMBA, JOSEPH OMOG.

KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog, amesema kuwa atalazimika kuongeza programu ya mazoezi, ili kuwajengea stamina wachezaji wake kwa lengo la kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoendelea kuanzia wiki ijayo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Omog, alisema kuwa lengo la kuboresha kikosi chake ni kutaka kukabiliana na ushindani ulioongezeka kwenye ligi hiyo baada ya kufanya tathmini ya mechi tano zilizopita.

Omog alisema kadri ligi inavyoendelea, ushindani pia unaongezeka kwa sababu kila timu inarekebisha makosa ambayo imeyabaini kwenye mechi zilizopita na kushuka uwanjani wakiwa imara zaidi.

“Timu zinaimarika kati ya mechi moja na mechi nyingine, na sisi tunahitaji kujiimarisha, ili tuweze kupata kile ambacho tunakihitaji, walioacha wakiwa wepesi, sasa wako tofauti, wamejifunza vitu vipya na wataingia uwanjani wakiwa na mbinu mpya," alisema kocha huyo.

Aliongeza kuwa, timu kufanikiwa kukaa kwenye uongozi wa ligi inahitaji nguvu ya ziada, lakini kuteremka ni suala "dogo".

"Kila mmoja lengo lake ni kukaa katika nafasi ya juu, ni ngumu kufika hapo na ni rahisi kuondoka, unapokuwa juu unaangaliwa na timu zote pinzani, kila mmoja anapambana kufika hapo tofauti na nafasi nyingine, tunahitaji kuongeza umakini, ili tusiipoteze nafasi hiyo muhimu na bora," alisema kocha huyo wa zamani wa Azam FC.

Aliongeza kuwa ushindani ambao wanaupata, mbali na kuwasaidia kufanya vizuri kwenye ligi hiyo, vile vile utawaandaa kupata matokeo mazuri kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika watakayoshiriki mwakani na Kombe la FA ambao wao ni mabingwa watetezi.

Simba ilitarajia kurejea jijini Dar es Salaam jana jioni ikitokea Dodoma na kuendelea na maandalizi ya kuikaribisha Mtibwa Sugar katika mchezo wa ligi utakaofanyika Oktoba 15 mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Hakuna maoni: