Jumapili, 1 Oktoba 2017
Haruna Niyonzima mashabiki mtafurahi tu
Kiungo wa Wekundu wa Msimbazi Haruna Niyonzima amewaomba mashabiki wa Simba waendelee kumuombea dua ili aweze kurudi katika ubora wake.
Niyonzima alijiunga na Simba msimu huu akitokea kwa watani wao, Yanga ambapo mpaka sasa hajafanikiwa kufunga bao tokea msimu ulipoanza, lakini amekuwa ni mchezaji anayependwa na kukubalika kwa mashabiki wa Simba.
“Nilikuwa katika kipindi kigumu kidogo cha kuzoeana na wachezaji wenzangu, lakini nafarijika sasa nimeanza kuzoea mazingira ndani ya Simba.
“Siku zote huwa naamini mimi ni mchezaji mzuri, lakini siwezi kuwa mzuri bila ushirikiano na wenzangu, hakuna mchezaji wa aina hiyo.
“Nimekuja Simba kufanya kazi, najua mashabiki wanatamani sana kuona ‘makeke’ yangu uwanjani, lakini wasiwe na wasiwasi siku si nyingi mambo yatakuwa mazuri,” alisema kupitia gazeti la Mwanaspoti.
Mchezaji huyo hata hivyo amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Simba licha ya kutofunga magoli. Emmanuel Okwi ndiye kinara wa mabao kwa Simba na Ligi Kuu Bara hadi sasa akiwa na magoli sita.
Leo jioni majira ya saa kumi kamili Simba Sc wanashuka dimbani kuvaana na Stand United katika dimba Kambarage Stadium ili kusaka pointi tatu muhimu.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni