KAYA takriban 39 wilayani Muleba mkoani Kagera hazina mahala pa kuishi, baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo ulioambatana na mvua kubwa ya mawe.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhandisi Richard Ruyango, alisema mvua hiyo ilinyesha Jumanne majira ya jioni na kusababisha maafa hayo.
Mbali na nyumba hizo kuezuliwa na nyingine kuanguka, pia mkuu huyo wa wilaya alisema mashamba yakiwamo ya migomba
yameharibiwa.
Alitaja maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo kuwa ni Kata ya Ibuga ambapo nyumba zilizoanguka ni 18, Kata ya Buganguzi nyumba 21 na kata ya Mubunda nyumba moja.
Kwa upande wake, Diwani wa Buganguzi, Fortunatus Mwebesa, alisema tathmini ya uharibifu inaendelea kufanyika kwa kushirikiana na wataalamu kutoka ngazi ya wilaya.
Mwebesa alisema pamoja na nyumba zaidi ya 20 kuezuliwa katika kata yake, pia chumba cha darasa katika Shule ya Sekondari Bukidea kimeezuliwa na nguzo tatu za umeme zimeanguka.
Ofisa Kilimo wa Kata ya Mubunda, Christopher Nicholaus, alithibitisha kutokea kwa uharibifu mkubwa kwenye mashamba ya migomba, na kuwa madhara makubwa yako katika Kijiji cha Kyaibumba.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya, taarifa kamili kuhusu maafa hayo itatolewa baada ya timu anayoiongoza kumaliza kazi ya tathmini, na mpaka sasa hakuna mtu aliyeripotiwa kujeruhiwa.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni