Habari rafiki msomaji wa mtandao huu,
Leo napenda tujifunze kuhusu wajibu wa serikali kwa wananchi, kumekuwa na dhana potofu kuwa wajibu wa serikali ni kuwafanyia wananchi kazi ili wapate mafanikio katika maisha yao. Wengine huenda mbali zaidi wakisema kuwa yapasa serikali iwajengee hata nyumba. Kiukweli huu ni uongo au dhana potofu na haitakuja kutokea serikali kumfanyia mwananchi maendeleo yake binafsi, au asije akaja mwanasiasa yeyote akakuahidi kuwa atakufanyia maendeleo yako wewe kama wewe hapo utakuwa umepotea kabisa hatimae utaishia kuilaumu tu na maisha yako yatazidi kudididmia tu katika dimbwi la umaskini!
By @zakaboyblog
Wajibu wa serikali ni kuhakikisha inatengeneza au kurahisisha upatikanaji wa maendeleo kwa wananchi unakuwa rahisi kwa kuboresha mifumo ya huduma mbalimbali ambapo mwananchi ambae atajituma sawasawa atafanikiwa kupitia huduma hizo na juhudi zake binafsi. Kama utalemaa hakika hakuna wokovu lelemama ambao utakuja ukukute umekaa.
Katika uchaguzi mkuu kila mtu anaetaka uongozi hufanya kampeni kwa kunadi sera zake ili apewe nafasi ya kuongoza nchi kwa kuboresha vipaumbele vyake kwa maslahi ya taifa na mengine aliyo na agenda nayo. Na si kweli kwamba serikali itakuja kwa Thomas Malale na kumjengea nyumba imfungulie biashara, kiukweli hicho kitu hakipo. Hebu tuangalie mifano ya huduma ambazo serikali inaweza kuzifanya na jinsi ambavyo zinaweza kukusaidia kuboresha maisha yako na kufikia mafanikio katika mtazamo sahihi na si ule wa kuletewa maendeleo hapo uliopo;
- Huduma za jamii; hapa ebu tuangalie baadhi ya hizo huduma. Kama serikali ikiboresha barabara si kwamba wewe mwananchi utaona moja kwa moja faida yake ila kuna faida wanaziita zisizo za moja kwa moja lakini ni muhimu sana katika mafanikio ya maisha yetu. Mfano kama wewe ni mfanyabiashara na usafirishaji wa bidhaa ndio hujenga asilimia kubwa ya biashara yako barabara itakuwa msaada kwako katika kufikia mafanikio yako kwa sababu; kwanza itakuwa inarahisisha usafirishaji wa bidhaa zako; pili, itasaidia kuokoa muda ambao ungekutumika mwingi kwa usafirishaji kwenye barabara mbovu; tatu, vyombo vyako vya kusafirishia havitapata hitilafu za mara kwa mara hivyo kuokoa fedha ambazo zingetumika kufanya marekebisho na kupelekea hasara. Vivyo hivyo kwa huduma zingine kama Afya na Elimu; kama kukiwa na huduma bora za afya zitasaidia mwananchi kutatua tatizo la magonjwa ambalo ni kikwazo katika shughuli zao za maendeleo, halihadhalika kwa elimu pia mwananchi anapopata huduma bora zinamsaidia yeye binafsi kuongeza maarifa yake yatakayo muongoza katika shughuli zake za maisha ambazo amejiwekea ili aweze kufikia mafanikio. Sasa kwa muktadha huu serikali haijakuletea maendeleo moja kwa moja nyumbani kwako bali imeboresha miundo mbinu ya wewe kufanikiwa, kazi inabaki kwako wewe mwananchi kujikwamua
- Huduma za kiuchumi; kama tulivyoona hapo juu hata katika huduma za kiuchumi serikali haileti maendeleo nyumbani kwako bali inaboresha mazingira yawe mazuri na ya kuvutia kwa wananchi kufanya biashara au shughuli zingine za kiuchumi. Mfano kama kuna sheria ambazo ni kikwazo kwa wananchi wazawa kuanzisha labda kampuni za huduma fulani ili wananchi waweze kunufaika serikali inaweza kufanya marekebisho ya sheria hiyo au kutunga nyingine ambayo itaendana na mahitaji ya wananchi wake ili waweze kuendelea kiuchumi. Pia inaweza kuboresha mahusiano na nchi marafiki ili kusaidia upatiakanaji wa masoko kwa bidhaa zinazozalishwa na wananchi, uboreshaji wa huduma za kibenki n.k. hapa serikali itakuwa imeboresha miundo mbinu ya uchumi hivyo wewe kama mwananchi jukumu lako ni kuchangamkia fursa tu ili upate kuyaona mafanikio na si kwa kulalamika kuwa serikali haisaidii mwananchi ilihali imekwisha fanya sehemu yake.
Naomba tuishie hapo mifano ipo mingi sana lakini lengo lilikuwa kukupatia taswira ya wajibu wa serikali na jinsi gani wewe kama mwananchi unaweza kufikia mafanikio yako kupitia wajibu wake huo. Labda kwa ufupi tu ni kwamba hatima ya maisha yako unayo wewe mwenyewe aidha uamue kufanikiwa ama kushindwa vyote vinatokana na uamuzi wako wewe mwenyewe. Hakuna mtu atakaekuja kukushika mkono na kukulazimisha kufanya kazi ili ufanikiwe. Na hivyo ndivyo ilivyo hata kwa serikali haimfati kila mmoja na kumwambia imfanyie nini ila hufanya kwa ujumla wote wanufaike na wale wanaolaumu kila siku serikali na kuishia kukaa tu wataendelea kufifia kimaendeleo badala ya kuchakarika na kazi. Zinduka Mtanzania, achana na dhana potofu!
By @zakaboyblog