Jumanne, 16 Januari 2018

Wizara nne kukabiliana na changamoto za utoaji huduma Uwanja wa Ndege Dar


SERIKALI, kupitia wizara zake nne, imedhamiria kukabiliana na changamoto mbalimbali za utoaji wa huduma kwa wageni wanaiongia na kutoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) wa jijini Dar es Salaam.

Changamoto hizo ni pamoja na msongamano na joto katika eneo la kuchukulia mizigo, muda mrefu wa upatikanaji wa hati za kusafiria kwa wageni wanaoingia nchini pamoja na changamoto ya ufinyu wa eneo la kusubiri huduma uwanjani hapo.

Mawaziri wa wizara hizo walifikia azimio hilo jana baada ya kufanya ziara ya pamoja katika uwanja huo na kukagua shughuli za utoaji huduma.

Mawaziri hao ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dk. Susan Kolimba na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye.

Akizungumza uwanjani hapo, Dk. Kigwangalla alisema amefikia hatua ya kukutana na mawaziri hao baada ya wageni, hasa watalii wanaiongia nchini, kulalamika kuwa wanatumia muda mwingi kuhudumiwa katika eneo la uwanja huo kiasi cha kuwapotezea muda.

Dk. Kigwangalla alisema kutokana na malalamiko hayo ya muda mrefu na mengine kadhaa, hatua mbalimbali zimechukuliwa tangu Agosti 8 mwaka jana wakati manaibu waziri wa wizara hizo nne walipofanya ziara uwanjani hapo.

Alisema kukutana kwao jana ni muelendezo wa kushughulikia kero hizo na kwamba mafanikio yameanza kuonekana.

Dk. Kigwangala alisema ipo haja ya kuweka mikakati ya kuboresha huduma katika viwanja vya ndege nchini, ukiwamo JNIA, na akasisitiza umuhimu wa watendaji na watoa huduma katika nafasi mbalimbali kuwa wakarimu kwa wageni.

Waziri huyo pia alisema ni vema polisi walioko uwanjani hapo kutotumia nguvu kukamata mgeni kwani ni muhimu kumdhibiti mgeni bila kutumia nguvu ili ikibainika hana kosa aachiwe na asiwe na malalamiko ya kunyanyaswa.

Dk. Kigwangalla alisema kuna haja kwa wageni wasimulie ukarimu na uzuri wa nchi yetu wanaporudi makwao.Waziri Kigwangalla alisema anatamani kuona kuanzia uwanjani hapo hadi hotelini ambako mgeni anakwenda, unatumika muda mchache.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Nchemba alisema jitihada mbalimbali zinafanywa kutatua changamoto hizo.

Alitaja hatua ambazo wizara yake inachukua kuwa ni kuharakisha utoaji huduma wa hati za kusafiria kwa njia ya kieletroniki.

“Taarifa zinaonesha kuwa kwa sasa kuna unafuu mkubwa wa kutoa huduma kwani badala ya saa tatu ambazo zilikuwa zinatumia awali hivi sasa muda wa utoaji huduma umeshuka hadi saa moja, lengo letu ni kushuka zaidi," alisema Waziri Mwigulu.

“Mbali ya kuboresha huduma tutahakikisha pia tunaongeza ulinzi na usalama katika viwanja vyetu vyote nchini ili kudhibiti wageni wenye nia ovu na nchi yetu."

Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Nditiye alisema wizara yake tayari imechukua hatua mbalimbali za kuondoa changamoto zilizopo ikiwamo ya kufunga viyoyozi kwa ajili ya kuondoa hali ya joto.

Hakuna maoni: