Jumamosi, 6 Januari 2018

Wenger apata mualiko kutoka kwa Weah

Rais mteule wa Liberia, George Oppong Weah amemtumia mwaliko kocha wa Arsenal, Arsene Wenger kuhudhuria tukio la kuapishwa kwake kama Rais mpya wa nchi hiyo.

Kocha huyo raia wa Ufaransa ambaye alimpokea Weah wakati akiwa kocha wa Monaco mwaka 1988 na kumfundisha hadi mwaka 1992 amesema ataangalia ratiba yake ya kazi kama itamruhusu kuhudhuria.

Hata hivyo nafasi pekee ya Wenger kwenda Liberia itategemea na hukumu ya FA ambayo inamkabili kocha huyo baada ya kukosoa maamuzi ya refarii baada ya mchezo kati ya Arsenal na Chelsea Jumatano iliyopita ambapo anaweza kufungiwa hadi mechi nne.

Weah anatarajia kuapishwa mwishoni mwa mwezi huu kwenye sherehe zitakazofanyika jijini Monrovia. Arsenal itacheza na Crystal Palace Januari 20 kwenye mchezo wa EPL pamoja na mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Chelsea Januari 24.

Hakuna maoni: