Wanafunzi wanaosoma katika shule za mikoa mbalimbali wamekwama katika kituo cha Mabasi cha Ubungo kutokana na matatizo ya usafiri.
Hata hivyo, Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra)ilisema imeshatoa vibali kwa ajili ya kuwasafirisha wanafunzi hao.
Wanafunzi hao tangu Desemba 2017 walikuwa likizo jijini Dar es Salaam na mikoa ya jirani baada ya shule kufungwa na leo walitakiwa kurudi shule.
Shule zinatarajia kufungua kesho Jumatatu Januari 8, 2017 na wanafunzi walionekana katika kituo cha mabasi cha Ubungo wakisubiri mabasi.
Wakizungumza ,na Mwananchi leo Januari 7 katika kituo cha mabasi ya Mikoani Ubungo (UBT) baadhi ya wanafunzi wamesema walifika kituoni hapo tangu juzi wakakosa usafiri hivyo wakajaribu tena leo bila mafanikio.
“Jana tulikuja hapa kutafuta usafiri lakini hatukufanikiwa tukarudi nyumbani, leo tumefika tena lakini hadi sasa bado hatujapata usafiri,” Hamida Masoud ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Mtakuja mkoani Manyara.
Alisema walitakiwa kuripoti shuleni tangu juzi ili kuwahi masomo yanayoanza kesho (leo) lakini usafiri umewakwamisha.
“Tunaomba serikali itusaidie tupate usafiri hata wa mabasi madogo ili tuwahi masomo,” alisema.
Mwanafunzi mwingine, Peter Kazimoto wa Shule ya Sekondari ya Umoja, mkoa wa Tanga amesema shule anayosoma ni ya kutwa na inafungua kesho.
“Hadi sasa (saa tano asubuhi) sijapata basi sijui kama nitawahi masomo kesho,” amesema.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano amesema wameshaanza kutoa vibali kwa wamiliki wa magari wanaotaka kusafirisha abiria mikoani.
“Tumeliona tatizo hilo jana na tumetoa vibali vya mabasi 43 kusafirisha wanafunzi, leo tumetoa vibali kwa mabasi 50 ili kuwasafirisha,” amesema.
Alisema hadi kufikia jana jioni ana uhakika wanafunzi wote na abiria wengine watakuwa wamepata usafiri kwenda katika mikoa mbalimbali nchini.
Amesema walitoa vibali kwa mabasi madogo yakiwemo ya daladala yenye sifa ya kuweza kusafirisha abiria katika umbali mrefu.
“Tumewaonya na tumewasisitiza kufuata sheria za usalama barabarani wakati wa kusafirisha abiria,” amesema.
Katika kituo hicho pia ilionekana misururu mirefu ya abiria waliojipanga kwa ajili ya kununua tiketi tofauti ya siku nyingine.
Misururu iliyotia fora ni ya mabasi yanayokwenda Morogoro, Kagera na Dodoma ambayo ilikuwa na abiria wengi kuliko wanaokwenda mikoa mingine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni