WAZIRI MKUU WA UINGEREZA THERESA MAY (KUSHOTO) AKIWA NA RAIS DONALD TRUMP WA MAREKANI. PICHA: MTANDAO
Aidha, imejikuta ikijiuliza maswali kama ina uwezo wa kustahimili adha za kisaikolojia za uendelezaji wa uhusiano huo.
Kilicholeta tatizo ni hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani kurusha upya katika ukurasa wake wa 'twitter' video iliyoandaliwa na kundi la 'BritainFirst' (Uingereza Kwanza) linaloendana katika hisia zake na kiongozi huyo wa Marekani, lakini linachukiwa na wahafidhina nchini Uingereza kuwa ni kundi la kifashisti.
Ni wazi kuwa utawala wa Uingereza chini ya Waziri Mkuu Theresa May unaendelea kuwakilisha hisia za wastani licha ya uhafidhina; haiwezi u-Trump wa sasa.
Video hiyo ilionyesha kijana (wa Kizungu) akitupwa nje ya chombo cha usafiri adhurike na watu ambao walisemekana kuwa ni wana-siasa kali, wakati tukio lenyewe halikuwa wazi ni la wapi, au ni mkanda wa kubuni tu kuzusha hisia kali.
Ndiyo utawala Uingereza ulivyoelewa suala hilo, kuwa video hiyo ni hatua tu ya propaganda ya kukosanisha hisia za watu na wafuasi wa dini nyingine, kujenga picha kuwa ni watu hatari - hivyo kuunga mkono vyama vya mrengo mkali wa kulia kuzuia uingiaji wa watu kutoka Mashariki ya Kati, n.k.
Ni video ambayo wafuasi halisi wa Trump nchini Marekani, wanaoitwa 'alternative right' (mrengo tofauti wa kulia, yaani mkali zaidi) wanaipenda, wanaamini hivyo, hata Trump akafuta uhamiaji kutoka nchi kadhaa.
Kinachoendelea nchini Uingereza hakitofautiani na kiongozi huyo wa Marekani katika maeneo yote, kwa mfano hatua ya wapiga kura Uingereza kuunga mkono azimio la kujitoa katika Umoja wa Ulaya, ambao sasa unaingia katika hatua za kukamilisha mkataba wa malipo maeneo tofauti yanayohusiana na kujitoa.
Hatua yenyewe ya Uingereza kutokuwa sehemu ya Umoja wa Ulaya inatazamiwa kukamilika mapema mwaka 2019, hivyo mwelekeo wa nchi hiyo unaendana na ule wa Rais Trump wa kuzuia Marekani kuendelea na mikakati ya kupanua utandawazi iliyofuatwa na tawala zilizopita nchini Marekani.
Hata hivyo, mwelekeo wa kihisia wa Trump unawakera wengi nchini Uingereza hata katika safu ya Baraza la Mawaziri la Theresa May, waziri mkuu.
Baadhi wamependekeza kuwa ziara ambayo kiongozi huyo wa Marekani anatazamia kufanya nchini Uingereza, licha ya kuwa ziara hiyo (mwezi haujatajwa) ni muhimu kwa Waziri Mkuu May kuhakikisha ana mikataba maalum ya kibiashara na Marekani wakati Uingereza inatoka rasmi katika Umoja wa Ulaya.
Hivyo kinachoonekana zaidi kisiasa ni jitihada za pande tofauti za kisiasa serikali ya Uingereza kurudisha umoja miongoni mwao, na kufaulu kuendeleza uhusiano maalum na Marekani, hasa kutafuta njia za pamoja za kupambana na makundi ya ugaidi yanayoipiga Ulaya kila mara, na Uingereza mara kadhaa sasa.
Baada ya May kupinga 'tweet' hiyo, Trump aliandika: kiongozi huyo alenge kupambana na ugaidi, si kumkosoa yeye.
Yako maeneo mengine ambako tofauti kati ya Uingereza na Marekani zinajionyesha katika maeneo kadhaa ambayo kimsingi ni muhimu zaidi kuliko propaganda za siasa kali kuhusu makundi ya vijana wenye madevu wakimtupa nje ya gari kijana wa Kizungu.
Kuna suala la kutambua jiji la Yerusalem kuwa mji mkuu wa Israel, hatua ambayo haijaungwa mkono na nchi hata moja nje ya Israel yenyewe, na hata nchini humo ni kundi la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na muungano wa vyama vya mrengo wa kulia ulioko madarakani ambao waliunga mkono.
Wengine, ikiwemo makundi kadhaa ya Wayahudi 'wapenda maendeleo' nchini Marekani walipinga hatua hiyo, wakisema inaongeza moto hisia za chuki kwa Israel, ambayo ilishateka, kutwaa mji huo.
Upande wa Magharibi wa Yerusalem, ulitekwa na kundi la wapiganaji wa Kiyahudi na kuwa sehemu ya Israel iliyoundwa mwaka 1947 na kutambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa mwaka uliofuata, wakati upande wa Mashariki ulitekwa na majeshi ya Israel katika vita vya siku sita vya mwaka 1967.
Umoja wa nchi za Kiarabu ambao wakati huo walijaribu kuunda nchi moja, yaani Misri, Syria na Jordan ulijaribu kupambana ili kuondoa uwepo wa Israel kama walivyokuwa wanataka tangu 1947 lakini wakashindwa, kwa Marekani kutoa msaada mkubwa wa upelelezi wa anga za juu za mpangilio wa majeshi ya nchi hizo yakielekea Israel.
Mpangilio huo ulipoharibiwa kwa mapigo mazito kutoka angani, uendelezaji wa misafara hiyo ya vifaru ukakwama, ukavia.
Uingereza bado iko katika mwelekeo wa kihisia na kidiplomasia kuwa kutotambuliwa kwa Yerusalem kama mji mkuu wa Israel ni kubakiza uwezekano wa kufikia amani kwa mfumo wa uwepo wa nchi mbili katika eneo hilo, kwa maana ya Palestina na Israel kutwaa pande mbili tofauti za mji huo.
Ni kutazamia kuwa Israel itarudisha mji huo kwa mazungumzo wakati hakuna mtaalamu wa usalama wa Israel anayeweza kuonyesha jinsi nchi hiyo inavyoweza kulindwa iwapo upande wa pili wa Yerusalem utakuwa mikononi mwa Wapalestina, na huku kinachodaiwa ni maafikiano kati ya Hamas na utawala wa Rais Mahmud Abbas utawezesha kundi hasimu la Hamas kuteka bila jasho Yerusalem Mashariki, maroketi yafute hamu ya Wayahudi kurudi, kuishi nchini humo.
Msingi wa amani ambao Waisraeli wanautambua ni kuendeleza hali iliyopo sasa, yaani Israel inajikuta eneo la Mashariki ya Bahari ya Kati (Mediterranean) hadi ukingo wa Magharibi wa mto Jordan, ili eneo hilo liweze kulindwa, tofauti na Yerusalem ikiwa chini ya mamlaka nyingine kisheria, kitaifa.
Halafu ina maana kuwa hata kama jamii za jadi (za Waarabu, ambao ni Waislamu pamoja na vikundi vidogo vya Wakristo) wataendelea kuwepo, wasiwe na uwezo wa kumiliki silaha au majeshi ambayo yanaweza kushambulia na kudhuru jamii za Kiyahudi.
Kwa mfano wale wanaokatiwa maeneo kujenga maskani ya Wayahudi katika eneo la Ukingo wa Magharibi ambalo kimsingi ni ardhi ya Wapalestina.
Mwaka 2000 maafikiano ya kurudisha ardhi hiyo nusura yafikiwe kati ya kiongozi wa Palestina Yasser Arafat na Waziri Mkuu Ehud Barak, katika mazungumzo ya Camp David nchini Marekani yaliyosimamiwa na Rais Bill Clinton, ila yakakwamishwa na suala la Yerusalem.
Arafat alikataa katakata kukubali kuundwa kwa nchi ya Palestina Ukingo wa Magharibi bila Yerusalem, ambayo Israel ilisema haiwezi kuiachia upande mmoja uwe wa Palestina, lakini watu wa dini zote waweze kutembelea maeneo yao matukufu ya kihistoria, kama Msikiti wa Al Aqsa kwa upande wa Waislamu.
Tangu wakati ule hadi sasa hali imebadilika sana Ukingo wa Magharibi na siyo rahisi chama chochote cha siasa nchini Israel kukubali shinikizo la Marekani (licha ya Umoja wa Mataifa) kuwa walowezi waondoke eneo hilo warudi Israel ya jadi, ile ya kabla ya vita vya mwaka 1967 kama inavyodaiwa katika busara ya 'suluhisho la kuundwa nchi mbili sambamba' katika eneo hilo hilo.
Kutambuliwa Yerusalem ni ishara kuwa hiyo ni ndoto.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni