Jumatano, 10 Januari 2018
Kamati maalum yakuishauri Serikali athari za bonde la Kilombero yatajwa
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangala, ameteua kamati maalum ambayo itaishauri Serikali namna ya nini kifanyike katika kushughulikia athari za bonde la Kilombero mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, Dk. Kigwangala amebainisha kamati hiyo aliyoiteua ndio itamshahuri juu ya bonde hilo, litasimamiwa vipi pamoja na namna bora ya hatua za kuchukua, ili kulinda bonde hilo ambalo lina mahitaji makubwa ikiwamo chanzo kikubwa cha maji yanayotengeneza Stiegler’s Gorge ambako Serikali imeamua kuweka mikakati ya utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme unaotarajiwa kufikia megawati 2,100.
Pia bonde hilo lina utajiri wa kuwapo na aina zaidi ya 400 ya ndege pamoja na mnyama aina ya puku ama sheshe ambaye hapatikani duniani kote zaidi ya Tanzania pekee.
“Hii ndio kamati yangu, itakayonishahuri juu ya bonde, ili litasimamiwa vipi. Hii ndio Kamati ambayo itanishahuri mimi na kwa maana hiyo Serikali kwa ujumla wake juu ya namna bora ya uhifadhi hususani katika eneo lile la pori tengefu.
Hapa kuna vitu viwili vya kuzingatia: Ardhi oevu (Ramsar site) ambalo lina eneo lake huku pia eneo la pori tengefu nalo kuchukua nafasi kubwa zaidi," alisema Dk. Kigwangala wakati wa kuteua kamati hiyo.
Kamati hiyo itaongozwa na Mwenyekiti Andrew Napacho na wajumbe ni Brigedia, Jenerali mstaafu Edmund Mndolwa, Kamishna mstaafu Suleiman Kova na Mwenyekiti Taifa wa Chama cha wafugaji, Semkae Kilonzo.
Wengine ni Dk. Simon Mduma, Prof. Jaffar Kideghesho, Ruzika Muheto, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, MKuu wa Wilaya ya Kilombero na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi.
Wengine ni Mwenyekiti wa Halmashauri Ulanga, Mwenyekiti wa Halmashauri Kilombero, Mwenyekiti wa Halmashauri Malinyi na Mwenyekiti wa Halmashauri Ifakara.
Pia yumo Mtendaji Mkuu wa KPL, Mtendaji MKuu wa Illovo, Mkuu Kikosi JKT Chita. Wengine ni Dk. Aggrey Mlimuka, Mwakilishi kutoka mamlaka ya maji Bonde la Kilombero, Mwakilishi kutoka Wizara ya Ardhi.
Wengine ni Innocent Kylogeris, Dk. James Wakibara na Mkurugenzi Mkuu TAWA ambaye atakuwa Katibu wa kamati hiyo.
Hatua hiyo inafuatia Waziri Kigwangala kufanya ziara maalum kwenye bonde hilo na kushuhudia athari kubwa zaidi zilizofanywa na wavamizi wakiwamo wakulima na wafugaji, ambao wameonekana kuvamia maeneo makubwa ndani ya pori tengefu la bonde pamoja na kwenye eneo oevu ndani ya bonde hilo.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni