SERIKALI imeanza kutumia mfumo wa nyota kupitia huduma zitolewazo na vituo vya afya, hospitali na zahanati ili kupima utendaji kazi wa watumishi wa sekta ya afya katika kutoa huduma kwa wananchi.
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile, aliyasema hayo alipotembelea Kituo cha Afya Nkomolo, Nkasi mkoani Rukwa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua shughuli za afya na uhamasishaji wa wananchi kujishughulisha katika shughuli za maendeleo.
“Tumeanza utaratibu wa kutoa nyota katika vituo vya afya inaanza nyota sifuri hadi tano, ambapo sifuri inamaana kituo hakifai kutoa huduma huku tano ikionyesha kinafaa kuendelea kutoa huduma,’’alisema.
Pia Dk. Ndungulile aliridhishwa na utoaji wa dawa katika kituo hicho na akawatoa hofu wananchi juu ya upatikanaji wa dawa kutokana na serikali kusema dawa zote zinapatikana katika vituo vya afya.
“Hatutarajii kuona mtu kaja kupata matibabu hapa halafu anaambiwa aende nje kununua dawa,’’alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy, aliupongeza uongozi wa mkoa huo kwa kusimamia vizuri ujenzi wa kituo hicho.
Alisema katika upande wa mochwali, wodi ya mama na watoto pamoja na ‘theater’ kiasi cha fedha kilichotumika ni Sh. bilioni 290 huku nguvu kubwa ya wananchi ikiwa imetumika.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Boniface Kasululu, alisema mkoa umeendelea kuboresha huduma za mama na mtoto. Alisema zaidi ya vituo 214 kati ya 223 vilivyopo vinatoa huduma muhimu za mama na mtoto jambo ambalo linasaidia kwa kasi kupunguza idadi ya vifo.
Pia alisema mkoa unaendelea kuwaelimisha jamii kuwapeleka wototo kupata huduma za chanjo.
Alisema Novemba, mwaka jana, zaidi ya watoto 40,000 wenye umri chini ya mwaka mmoja, walipatiwa chanjo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni