Jumatano, 10 Januari 2018

Ndugulile atoa agizo kuhusu afya

Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile imeviagiza vyombo vya usalama na Kamati za Afya za vijiji kuimarisha mifumo yote ya udhibiti wa upotevu wa dawa nchini.

Naibu Waziri ameyasema hayo kwenye ziara yake wilayani Uvinza Mkoani Kigoma, ambapo amesisitiza vyombo hivyo kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba, ili kuondoa ubadhilifu unaofanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Ndugulile amekagua utoaji wa huduma za Afya na kufuatilia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya jamii ambayo inasisitiza ushirikishwaji wa jamii katika maamuzi.

Ndugulile ameongeza kuwa serikali imewekeza kiasi cha Shilingi Milioni 400 katika Halmashauri 175, kikiwemo kituo cha Afya cha Uvinza, fedha zitakazotumika kuboresha na kujenga vyumba vya kutolea huduma ya dharura wakati wa kujifungua, nyumba za watumishi pamoja na maabara.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania imeongeza bajeti ya dawa, kutoka bilioni 30 hadi bilioni 270 kwa mwaka huu wa fedha, hali iliyosaidia kuimarisha mapambano dhidi ya maradhi mbali mbali.



Hakuna maoni: