Alhamisi, 11 Januari 2018

Mashindano ya UVCCM yazinduliwa rasmi leo

Mashindano ya UVCCM Cup kata ya Mzimuni Magomeni yamefunguliwa leo na Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kinondoni, Themed Salim  ambapo yatashirikisha Timu 16 huku mshindi wa kwanza akijinyakulia kitita cha Sh Laki mbili na jezi seti moja, wa pili akipata jezi seti moja na Sh Laki moja na wa tatu akipata Sh 70,000.

Mchezo wa kwanza leo ulizikutanisha Timu za Maveterani FC dhidi ya Bayern Munichen ambapo ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2. Magoli ya Munichen yalifungwa na Pascal Thomas dk 13 na Salum Ramadhan dk 29 ya kipindi cha kwanza kabla ya Abdul Maneno kuisawazishia Maveteran dk ya 20 kipindi cha pili na baadaye Ochu akaiandikia Timu hiyo bao la pili dk 24 ya kipindi cha pili.

Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika Muandaaji wa Mashindano hayo ambaye ni Mwenyekiti wa UVCCM kata ya Mzimuni, Abdallah Mwakilima alisema lengo la mashindano hayo ni kujenga ushirikiano na umoja pamoja na kuongeza utimamu wa mwili kwa vijana wa kata hiyo.

" Nashukuru muitikio wa watu umekuwa mkubwa uwanjani leo lakini niwaombe mashabiki wazidi kujitokeza kwa wingi kwenye kila mchezo ili kuweza kuwasapoti vijana wetu. Lengo la mashindano haya ni kujenga umoja na kukuza vipaji vya wachezaji ambao wako mitaani, tunaamini kupitia mashindano haya vipaji vingi vitaonekana. Niwaombe watu wa kada mbalimbali kujitokeza na kutupa sapoti yao," alisema Mwakilima.

Mashindano hayo yataendelea kesho jioni kwa mchezo kati ya Timu ya Watu Hatari dhidi ya Immigration katika uwanja wa Uweje Juu.

Hakuna maoni: