Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh6 milioni, wafanyabiashara wawili, Naushad Mohammed Suleiman (63) na Ali Makame Juma (36) baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha vipande saba vya madini ya dhahabu vyenye thamani ya Sh 989.7 milioni bila kuwa na leseni.
Pia, mahakama hiyo imetaifisha dhahabu yote iliyokamatwa pamoja na mabegi mawili ya fedha mbalimbali kutoka nchi 15 duniani, walizokamatwa nazo, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aman Karume uliopo Zanzibar.
Hukumu hiyo imetolewa jana Alhamisi, Januari 11 na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya washtakiwa hao kukiri mashtaka yanayowakabili.
“Ili iwe fundisho kwa watu wengine, katika kosa la kwanza mahakama inawahukumu kulipa faini ya Sh.milioni 2 ama jela miaka 2, pia kosa la pili faini Sh.mil 4 ama jela miaka 3, mkishindwa mtaenda jela na kutumikia vifungo hivyo sambamba,” Alisema Hakimu Mashauri
Wafanyabiashara hao maarufu ambao ni wakazi wa Zanzibar, walikuwa wanakabiliwa na makosa mawili, ambayo ni kula njama na kusafirisha madini nje ya nchi kinyume cha sheria na bila kuwa na leseni kutoka mamlaka husika.
Washtakiwa wanadaiwa kukamatwa Novemba 29, 2017, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aman Karume, wakisafirisha madini hayo kwenda Dubai katika Falme za Kiarabu.
Hata hivyo, wafanyabiashara hao walilipa faini na kuepuka kifungo hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni