WATU watatu wamekufa papo hapo na wengine 14 kujeruhiwa, kutokana na ajali iliyotokea jana (juzi) katika kijiji cha Machazo, Kata ya Simbo mkoani Kigoma.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kigoma ya Mweni, Dk. Fadhili Kibaya, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo huku akikiri kupokea jana asubuhi maiti tatu na majeruhi 14.
Dk. Kibaya alikanusha taarifa kuwa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni wanane.
"Sijapokea maiti nane, acha wananchi waseme lakini mimi nimepokea maiti tatu na majeruhi wanawake wanne, wanaume wanane na watoto wawili ambao wanahudumiwa hospitali ya Maweni," alisema Dk. Kibaya.
Naye Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Sweetbert Njowike, aliiambia Nipashe kwa njia ya simu kuwa ajali hiyo, ilitokana na basi dogo aina ya Toyota Hiace na Mitsubishi Fuso.
Alisema Toyota Hiace yenye namba za usajili T142 CKU iliyokuwa imebeba abiria kutoka Kasulu kwenda Kigoma mjini kugongana na Fuso yenye namba za usajili T288 ASC katika kijiji cha Machazo saa 3:40 usiku.
Kamanda Njowike alisema magari hayo yaligongana na kusababisha watu watatu kufariki dunia papo hapo huku wengine 14 wakijeruhiwa.
"Chanzo cha ajali ni dereva wa Hiace kugonga Fuso iliyokuwa imepaki pembeni, ni dereva wa Hiace alikosea hesabu,” alisema Kamanda Njewike.
Kamanda huyo alisema pamoja na dereva wa Hiace kuvunjika mguu wa kulia, anashikiliwa na polisi kwa kusababisha ajali hiyo na kwamba anatarajiwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria baada ya taratibu kukamilika.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni