Jumatano, 10 Januari 2018

Kikao cha Magufuli, Lowassa Ikulu chazua mshangao

Ni mshangao. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais John Magufuli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kufanya mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam jana, lakini kwa sasa walichokizungumza kinabakia kuwa siri ya wawili hao.

Hakuna aliyedhania wala kutarajia kuwa hilo lingetokea, hasa katika kipindi hiki chenye matukio mengi ya kutuhumiana kati ya viongozi wa upinzani na Serikali.

Lakini, jana ilikuwa mara ya kwanza kwa viongozi hao kufanya mazungumzo tangu Lowassa alipojiengua CCM na ya kwanza tangu kumalizika Uchaguzi Mkuu uliopambanisha wawili hao na uliokuwa na ushindani kuliko wakati mwingine wowote tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani.

Lowassa alimsifu Rais Magufuli kwa kazi anazoendelea kuzifanya, ikiwa ni pamoja na miradi ya maendeleo, elimu na ajira na pia mkuu wa nchi akamsifia mbunge huyo wa zamani wa Monduli kwa kuendesha siasa za kistaarabu.

Lakini kauli ya Lowassa ilikosolewa mara moja na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye alisema “unahitajika ujasiri sana kuisifu Serikali” kutokana na masuala ya kuminywa kwa demokrasia, uchumi kuporomoka, watu kutekwa na wengine kutoweka, akisema sifa hizo si kauli za chama hicho kikuu cha upinzani.

Kauli ya Mbowe pia iliungwa mkono na wanasiasa wengine na wachambuzi ambao licha ya kusema Lowassa ana haki hiyo ya kuonana na Rais, lakini walisema aliyoyasema ni maoni yake.

Mazungumzo ya wawili hao yameacha mshangao na mjadala mkubwa mitandaoni.

Mara ya kwanza viongozi hao walikutana Agosti 28, 2016 ikiwa ni miezi 16 tangu Lowassa alipohamia Chadema kupinga mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM ulioisha kwa Magufuli kupitishwa.

Siku hiyo walikutana kwenye misa ya shukrani ya kuadhimisha miaka 50 ya ndoa ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa iliyofanyika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Jana, picha za video zilizotumwa na mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa zinamuonyesha Magufuli akimpokea Lowassa, baadaye zinawaonyesha wakiwa katika mazungumzo kabla ya picha zinazowaonyesha wakitoka na kusimama kuzungumza na waandishi.

Lowassa afarijika

Wote wawili walisema waliongea masuala mengi, lakini Rais akasema hawezi kuyaeleza yote.

“Kwanza nimepata faraja sana kuja Ikulu,” akasema Lowassa.

“Nimepata nafasi nzuri ya kuzungumza naye na kwanza kumpongeza kwa kazi nzuri anayoifanya. Anafanya kazi nzuri inayoonekana na anahitaji kutiwa moyo.

“Tumezungumza vizuri, tumekumbushana mambo mengi, tumeelewana vizuri. Nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya. Kubwa ambalo halimsemi sana ni la kujenga ajira.”

Lowassa alisema ujenzi wa reli kwa ajili ya treni ya umeme na mradi wa umeme wa Stieglers Gorge utazalisha ajira kwa wengi pamoja na suala la elimu bure.

“Wanasema wazungu he has made my day, ameifanya siku yangu kuwa njema sana. Mazungumzo yangu na yeye yamenipa faraja kubwa sana,” alisema Lowassa.

Magufuli amsifu Lowassa

Rais Magufuli naye alimmwagia sifa mpinzani wake huyo katika uchaguzi uliopita.

“Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane naye, na leo (jana) nimekutana naye. Tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu,” taarifa ya Msigwa inamkariri Rais Magufuli.

“Mzee wetu, Mzee Lowassa ni mwanasiasa mzuri na kama mnavyofahamu ana historia nzuri katika nchi hii,” anasema Rais Magufuli katika mkanda wa video uliotumwa baadaye na idara hiyo.

“Na kikubwa zaidi ambacho nampongeza Mheshimiwa Lowassa tofauti na wanasiasa wengi, wakati wa kampeni zote za urais, Mheshimiwa Lowassa hakuwahi kutamka hata neno moja la kunitukana, hata la kutukana hakuwahi. Tafuteni mahali popote ambapo alitukana, ukiachia wale wapambe wake ambao nina uhakika hakuwatuma.”

Na Lowassa kujibu hakuwatuma.

“Wale ndio waliokuwa wanaropoka. Amefanya siasa za ustaarabu na ndio maana mimi nampongeza, namtakia mafanikio mema,” alisema Rais.

“Na mimi kama Rais, kama kiongozi wake, nitaendelea kutoa ushirikiano mkubwa sana kwa mheshimiwa Lowassa.”

Alisema mbunge huyo wa zamani wa Monduli amefanya mambo mengi na amezungumza mengi, ikiwa ni pamoja na kushauri, lakini hangeweza kuyasema yote na Rais pia akazungumza yake.

“Kwa ujumla Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri na mimi napenda kumpongeza Lowassa ambaye kama alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi,” alisema.

Kwa sasa, Lowassa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, chama ambacho kinapinga vikali uendeshaji nchi wa Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano, huku viongozi wa upinzani wakikamatwa mara kwa mara na baadhi kufunguliwa kesi.

Lowassa ameshakumbana na misukosuko hiyo, ikiwa ni pamoja na kuitwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuhojiwa zaidi ya mara tatu, akidaiwa kutoa maneno ya uchochezi katika futari iliyoandaliwa na mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara.

Katika futari hiyo, Lowassa alimtaka Rais Magufuli kuwaachia huru masheikh wa kikundi cha Uamsho wanaoshikiliwa kwa zaidi ya miaka minne sasa.

Lowassa alijiunga na Chadema Julai 28 mwaka 2015 na baadaye kupewa fursa ya kugombea urais akiungwa na vyama vingine vitatu vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Katika uchaguzi, Lowassa alivuta hisia za wengi na kuweka upinzani mkubwa kwa Magufuli, ambaye hatimaye alishinda kwa tofauti ndogo ya kura kulinganisha na chaguzi zilizopita. Alipata kura milioni 8.8 wakati Lowassa alipata milioni 6.07.

Pamoja na kutoka, Lowassa amekuwa akitajwa mara kwa mara kwenye vikao vya juu vya CCM na baadhi ya wanachama waliotimuliwa kutokana na kuendelea kumuunga mkono wakati wa kampeni za uchaguzi huo.

Source: Mwananchi

Hakuna maoni: