Jumatano, 10 Januari 2018

kampuni za simu, Benki zitakazokaidi mfumo wa kielektroniki kufutiwa leseni


Dar es Salaam. Serikali imeziagiza benki zote 58 na kampuni saba za mawasiliano kujiunga na mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato kupitia kituo cha data kilichopo Kijitonyama jijini hapa vinginevyo zitanyang’anywa leseni ya biashara hivyo kukosa uhalali wa kuendesha shughuli zao nchini.

Agizo hilo lililotolewa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipokutana na viongozi wa benki 20 ambazo bado hazijajiunga kwenye mfumo huo na kuzipa hadi Januari 31.

“Huu ni utekelezaji wa kanuni ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi mwaka 2017 inayozitaka benki za biashara na kampuni za simu kujiunga na mfumo huo kati ya Juni, hadi Desemba 2017 lakini mpaka sasa ni benki 27 tu zimetekeleza hatua hiyo ya kisheria,” alisema.

Kwenye mkutano wake na viongozi wa benki hizo, waziri Mpango alisema amebaini sababu kadhaa ikiwamo hofu ya wizi wa mtandaoni, ughafla wa utekelezaji wa kanuni hizo kwa benki kubwa kama City Bank yenye matawi kwenye takribani nchi 100 duniani kote hivyo kuwalazimu kuwasiliana na makao makuu kabla ya kufanya utekelezaji.

Waziri anatekeleza agizo alilopewa na Rais John Magufuli Desemba 20 mwaka jana wakati wa uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mjini Dodoma.

Sheria ni msumeno, pamoja na sababu za msingi zilizopo, benki hizo zimeenda kinyume na utaratibu uliopo. Kutokana na ukweli huo kwamba hazijatekeleza sheria hiyo kwa miezi saba iliyotolewa, Waziri Mpango amemuagiza Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere kuwachukulia hatua za kisheria ikiwamo kuwatoza faini katika kipindi walichoshindwa kutekeleza agizo hilo.

Wakati zilizoshindwa zikiadhibiwa, Dk Mpango amezipongeza taasisi zilizotekeleza sheria ndani ya muda uliowekwa. Amezitaja benki zilizofanya hivyo kwa wakati kuwa ni Exim, CRDB, NMB, Stanbic na DTB.

Nyingine ni Benki ya Posta, Amana, China Commercial Bank, Akiba Commecial Bank na I&M. kwenye orodha hiyo, zimo pia Benki ya DCB, Benki ya Mkombozi na Benki ya Maendeleo.

Miongoni mwa benki alizozungumza nazo jana ni Bank of Africa (BoA), Yetu Microfinance Bank, Barclays na Benki ya Wananchi.

Kuhusu mwenendo usioridhisha wa sekta ya fedha nchini hasa kuongezeka kwa mikopo isiyolipika, Waziri Mpango alikiri kuwa hali haikuwa nzuri mwaka jana kwa kuwa wastani wa mikopo hiyo ulifikia asilimia 12 ya yote iliyotolewa na taasisi hizo ingawa sasa mambo yameanza kubadilika.

“Benki Kuu ipo imara na sekta ya benki kwa sasa ina ukwasi wa kutosha. Kwa sasa wadau wanaona tupo katika hatua nzuri katika eneo hilo,” alisema.

Kujidhatiti na mabadiliko yanayoweza kujitokeza, waziri alizishauri benki kuwa na mfumo mzuri unaofuata taratibu za mikopo kwa kukopesha watu wenye vigezo.

Hakuna maoni: