Ijumaa, 19 Januari 2018
Kenyatta kuchukua hatua kuzima uasi Jubilee
Nairobi, Kenya. Rais Uhuru Kenyatta ameamua kuchukua hatua kuzima uasi uliomo ndani ya chama cha Jubilee akiwataka wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kuwaondoa wenyeviti waliochaguliwa kuongoza kinyume cha matakwa yake.
Wenyeviti wanaotakiwa kuondolewa ni Alfred Keter (Nandi Hills), anayeongoza Kamati ya Ajira; Silas Tiren (Moiben) wa Kamati ya Kilimo; Kangogo Bowen (Marakwet Mashariki) wa Mazingira na Rasilimali, na James Gakuya (Embakasi Kaskazini) Utangazaji na Maktaba.
Uamuzi huo ulifikishwa wakati wa kikao cha pamoja kati ya wabunge wa kamati hizo nne na Rais Kenyatta kilichofanyika Ikulu.
Wabunge hao wanne wamekuwa wakizozana na viongozi wa Jubilee ndani ya Bunge tangu walipojitokeza kwenda kinyume na matakwa ya rais na kuchukua mkondo wao wa utendaji kazi katika kamati.
Hata hivyo, katika kikao hicho cha Alhamisi, Keter na Tiren walibaki wakaidi wakisisitiza kwamba walichaguliwa kihalali kama wenyeviti na wakaapa kuendelea kushikilia nafasi zao hivyo kuzidi kutatiza mambo ndani ya Jubilee.
Keter, ambaye amejitokeza kuwa kinara wa waasi na ambaye anajivunia ukweli kwamba alichaguliwa tena licha ya kupingwa na Jubilee katika kipindi cha kwanza, aliwaelezea wenzake kuwa “vibaraka wa serikali na wanaoharibu uhuru wa Bunge”.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni