Alhamisi, 18 Januari 2018
Anusurika Kifo akipambana na Mamba kwa zaidi ya saa moja
MKAZI wa Kijiji cha Mkombe Kata ya Kabwe wilayani Nkasi, John Mwipungi (30), amenusurika kifo baada ya kupambana na mamba kwa zaidi ya saa moja.
Mwipungi akikumbana na mkasa huo alipokwenda mtoni kunawa miguu baada ya kutoka shambani.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 11 baada ya Mwipungu kufika mtoni kisha kuanza kunawa miguu kutoa tope baada ya kutoka katika shamba lake alikokuwa aking’oa majani katika mpunga.
Diwani wa Kabwe, Asante Lubisha, alisema majeru huyo alifika mtoni hapo na kuanza kunawa huku akiwa ameinama bila kuona kama kuna mamba katika eneo hilo.
Alisema wakati akiendelea kunawa miguu, ghafla aliibuka mamba mkubwa na kumvutia ndani ya mto, lakini kwa kuwa alikuwa anajua kuogelea alipambana naye ndani ya maji.
Alisema ujuzi wa kuogelea ulimsaidia Mwipungi kwa sababu aliamua kuvutana na mambo huyo eneo ambalo lina kina kirefu, hali iliyosababisha mamba huyo kushindwa kumuua na ilichukua saa nzima kupambana majini huku akipiga kelele za kuomba msaada.
Diwani huyo alisema Mwipungi alijeruhiwa na mamba huyo katika mguu wake wa kulia.
Aliongeza kuwa kutokana na kelele alizokuwa akipiga za kuomba msaada, wanakijiji walifika na kumtoa majini akiwa amejeruhiwa kisha kumkimbiza katika Zahanati ya Kabwe kupatiwa matibabu ya jelaha la mguu.
Diwani huyo alisema wananchi wamekuwa wakiuawa na mamba katika mto huo na kuwa mwaka jana mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kabwe wa darasa la sita aliliwa na mamba wakati akivuka katika mto Mkombe.
Alisema Kijiji cha Kabwe kimapakana na Pori la Akiba la Lwafi, hali inayosababisha wanyama wa hatari kama mamba, tembo, viboko na nyati kuingia kijijini hapo, hivyo kuhatarisha maisha ya wakazi wa kijiji hicho.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kabwe, Gwira Aron, alisema majeruhi huyo alipatiwa matibabu na anaendelea vizuri.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni