Jumamosi, 30 Desemba 2017

TANROAD YAVUNJA MSIKITI KIMARA

Maofisa wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wakiwa na polisi jana walibomoa Msikiti wa Al Kirumbi uliopo Kimara Mwisho ambao waumini wake waligoma kuubomoa kwa maelezo kwamba imani yao hairuhusu.

Habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema hilo limewezekana baada ya Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir kutuma ujumbe kupitia kwa msaidizi wake, Sheikh Issa Khalifa Issa kuwasihi waumini hao kutii amri ya Serikali kwa kuondoa kila kilichokuwamo ndani ya msikiti kama vitabu vya dini, mazulia, jeneza na spika.

Msikiti huo ni miongoni mwa nyumba 33 za ibada ambazo pamoja na vituo vya mafuta, afya na ofisi za Serikali zitabomolewa muda wowote baada ya kumalizika kwa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Nyumba hizo na nyingine takriban 2,000 za watu binafsi zinadaiwa kujengwa ndani ya hifadhi ya Barabara ya Morogoro kuanzia Kimara Mwisho hadi Kiluvya ambayo ni mita 121.5 kutoka kila upande. Mpaka sasa nyumba zipatazo 1,000 zimebomolewa na nyingine zaidi ya 1,300 zilizowekwa alama ya X Novemba 22, zinatarajiwa kubomolewa hivi karibuni.

Kuhusu msikiti huo, imeelezwa kwamba awali, maofisa wa Tanroads walifika hapo Oktoba 16 kwa lengo la kuubomoa lakini walishindwa baada ya waumini kugoma kuondoa vitu vilivyokuwamo ndani ya msikiti huo kwa madai kuwa imani yao haiwaruhusu kufanya hivyo.

Imamu wa Msikiti huo, Ramadhani Juma alisema ni mwiko na ni kosa kubwa kwa muumini wa Kiislamu kushiriki kubomoa nyumba ya Mungu wala kuhamisha kitu chochote kilichomo ndani, msimamo ambao uliwafanya maofisa hao kuondoka bila kufanya chochote huku wakiwapa wiki nne wawe wamefanya hivyo.

“Nawaomba waumini wenzangu, mimi nimetumwa na Mufti anaomba mruhusu Serikali ifanye kazi yake, jambo la msingi tafuteni eneo mkishapata tutashirikisha na Serikali na wahisani wengine watusaidie kujenga msikiti mwingine,” alisema Sheikh Issa.

Baada ya kusema hivyo Imamu wa msikiti huo kwa kushirikiana na waumini wake waliondoa baadhi ya vifaa na msikiti huo ukabomolewa.

“Tumekubali maana wamesema Serikali itatusaidia kufanya harambee ya ujenzi wa msikiti na sisi tumekubali kwa mikono miwili,” alisema Imamu Juma.

Mmoja wa maofisa wa Tanroads aliyekuwapo katika eneo hilo ambaye hakutaka kutajwa jina kwa kuwa si msemaji, alisema wanaendelea na ubomoaji.

“Tumeanza na huu msikiti wa Kirumbi, tunaendelea na misikiti mingine. Leo tunabomoa nyumba zote za ibada zilizosalia ili kumaliza kabisa,” alisema.

Bomoabomoa nyingine

Wakati msikiti huo ukibomolewa jana, Tanroads inadaiwa pia kuweka alama mpya za X juzi kwenye nyumba nyingine tano eneo la Kimara Mwisho. Imeelezwa kwamba nyumba hizo ziliachwa kwa makosa wakati wa tathmini ya uwekaji wa alama ya awamu ya kwanza ikidaiwa kuwa ni kutokana na wamiliki wake kuhamisha mawe ya alama za mwisho wa barabara.

Ofisa mwingine wa Tanroads ambaye pia aliomba jina lake lihifadhiwe alisema: “Ni kweli tumeweka alama hizo juzi kwa nyumba ambazo wamiliki wake walikuwa wamehamisha mawe yanayoonyesha mwisho wa barabara.”

Hata hivyo, wamiliki wa nyumba hizo walikana kuhamisha mawe hayo wakisema eneo hilo limekuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi na Serikali. Walisema wanaiona hatua hiyo kama ni kuwakomoa.

“Haya mawe wanayosema wakati mimi ninajenga hapa yalikuwa yameishia pale (alionyesha mita chache kutoka ilipo nyumba yake) unaona bwana! Sasa mimi nimeondoaje hayo mawe?” alihoji mmoja wa wenye nyumba hao, Salum Hamis.

Mmiliki mwingine, Silvester Mwasha alisema: “Kweli walikuja jana (juzi) wakapima tukashangaa tunawekewa X. Tulipohoji wakasema walikosea kupima mara ya kwanza sababu kipimo walichotumia hakikuwa na uwezo mzuri.” Mmoja wa wapangaji katika moja ya nyumba zilizowekewa X, Anne Majura alisema anashangaa baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo hawakushtuka maofisa hao wa Tanroads walipokwenda kuweka X.

Source: Mwananchi



Hakuna maoni: