Kutokana na tukio la wanafunzi watatu wa shule ya sekondari Ndyuda iliyopo mji mdogo wa Mlowo wilaya ya Mbozi kufariki kwa kupigwa radi, jeshi la polisi mkoani Songwe limewataka wananchi kutohusisha tukio hilo na imani za kishirikina na kushauri jamii kuchukua tahadhali kwa kuepuka mazingira hatarishi hususani katika kipindi hiki ambacho mvua kubwa zinanyesha maeneo mbalimbali zikiambatana na radi.
Akizungumzia tukio hilo Mrakibu Mwandamizi wa polisi kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Songwe Yusufu Sarungi amewataja watoto 3 waliofariki dunia kutokana na ajali ya radi iliyopiga wakati mvua zikinyesha jioni ya jumatatu hii kuwa ni Haruna Mwashiuya (15) Ashley Kalinga (13) na Godfrey Nzowa (13) wote walikutwa na kadhia hiyo walipokuwa wakicheza mpira.
Sarungi amesema jeshi la polisi limepokea taarifa hizo kwa masikitiko lakini akatahadharisha vifo vya wanafunzi hao kutohusishwa na imani za kishirikina zinazoweza kupelekea miongoni mwa wananchi kujichukulia sheria mkononi na kuhatarisha amani.
Mkuu wa shule ya sekondari Ndyuda Christopher Kafuru ametajwa kusikitishwa kwake na tukio hilo akidai kuwa limetikisa utulivu wa watahiniwa wa kidato cha nne wanaoendelea na mitihani ya taifa shuleni hapo, huku wazazi wakiwashauri walimu kuhakikisha wanafunzi wanapewa uangalizi wa kutosha wakati mvua kubwa zikinyesha.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni