Wananchi wa vijiji mbalimbali vya wilaya ya Kilwa mkoani Lindi wameiomba serikali kuingilia kati na kuchukua hatua za haraka kuondoa tatizo la ongezeko la mifugo ambayo imeanza kusababisha migogoro mikubwa na uvunjifu wa amani.
Wananchi hao wamesema kuwa vijiji vingi katika wilaya ya Kilwa kikiwemo kijiji cha Ngea havina maeneo kwaajili ya mifugo lakini wafugaji wamekuwa wakiingia na makundi ya mifugo na kuchunga mashambani na kwenye misitu ya vijiji na kusababisha kukauka kwa baadhi ya vyanzo vya maji na uharibifu wa mazingira.
Baadhi ya wafugaji waliokutwa na makundi ya mifugo wakiwemo ndama wengi wakihama kutafuta maeneo yenye malisho wamesema wamekuwa wakisumbuka na kutangatanga bila mafanikio tangu waliopohamishwa katika bonde la Ihefu wilayani Mbarali mkoani Mbeya mwaka 2006 na wengine wamesema wametoka Dodoma kwenda mkoani Lindi kutafuta malisho lakini hawana vibali vya kuhamia katika mkoa huo.
Akizungumzia changamoto hiyo ya mifugo Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Christopher Ngubiagai amesema Wilaya hiyo mpaka sasa ina Ng'ombe zaidi ya 40,000 waliosajiliwa na suluhisho la kumaliza migogoro hiyo ni zoezi la upigaji chapa na utambuzi wa mifugo kwenye vijiji mbalimbali unaotarajiwa kukamilika kabla ya desemba 31 mwaka huu na amewataka wafugaji kutoingia kwenye vijiji ambavyo havijapangiwa kupokea mifugo.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni