Monrovia, Liberia. Makao makuu ya chama tawala cha Unity (UP) yaligubikwa na vurugu mwishoni mwa wiki baada ya vijana wenye hasira wa tawi la chama kushinikiza Rais Ellen Johnson Sirleaf afukuzwe.
Vijana walitoa wito wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya UP kufanya uamuzi wa kumfukuza Rais Sirleaf.
Kwa mujibu wa vijana hao, Rais Sirleaf haonekani kujikita katika kukiimarisha chama na kwamba matendo yake yanakidhoofisha hasa katika wakati huu muhimu wa maandalizi ya uchaguzi mkuu.
"Tunataka Rais Sirleaf afukuzwe haraka kutoka kwenye chama tunachokipenda. Kwa sasa hana msaada kwenye chama na kwa hiyo hatumhitaji. Tusikae hapa na kumruhusu mwanamke huyu aharibu taasisi yetu,” Emmanuel James aliyejitambulisha kuwa mjumbe wa tawi la vijana la UP aliliambia gazeti la Daily Observer Jumamosi.
Alisema huruma ya chama kwa rais huyo anayestaafu imempa nafasi kubwa ya kukijeruhi chama, kama inavyoonekana sasa. Alisema kama hatua madhubuti zingechukuliwa dhidi yake, kama ilivyokuwa imependekezwa na baadhi ya maofisa, UP isingejikuta katika hali hii ya kusikitisha.
"Tumekuwa wapole sana na Rais huyu na matokeo yake ndiyo haya. Nadhani ingekuwa busara kama tungeanza nay eye kwa kuchukua uamuzi mgumu kama walivyopendekeza wengine,” alisema James.
Hata hivyo, makamu mwenyekiti wa UP J. Emmanuel Nuquay aliingilia kati na kutuliza vijana wenye hasira na akawaahidi kwamba takwa lao litaangaliwa na kwamba hakuna haja ya kuzua zogo. Alisema UP imejiandaa kwa wakati wa kihistoria nchini na kwa hiyo hakuna sababu ya kuvuruga mambo.
"Nimesikia kile ambacho mnasema na tunawahitaji mtulie wakati huu tunaposhughulikia mambo kadhaa,” alisema.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni