Jumapili, 26 Novemba 2017

Polisi yatawanya 'wafuasi' wa Chadema kwa mabomu

Polisi wilayani Malinyi wamelipua mabomu ya machozi kusambaratisha wananchi waliokua wanasogelea kituo cha kuhesabia kura cha Shule ya Msingi Sofi.

Akizungumzia hali hiyo leo Jumapili jioni, msimamizi wa uchaguzi wilayani humo Marcellin Ndimbwa amesema wakati zoezi la kuhesabu kura lilipoanza kuna vijana wa Chadema walisogelea kituo cha kuhesabia kura wakitaka kuleta fujo ndipo wasimamizi walipoomba msaada wa polisi.

"Kuna vijana wa Chadema wametoka wilaya jirani ya Kilombero ndio wanaotaka kuleta fujo ila wamedhibitiwa na hali ni shwari," amesema Ndimbwe.

Msimamizi huyo amesema zoezi la kuhesabu kura katika kata hiyo ya Sofi  linaendelea vizuri.

Hata hivyo, madai hayo ya vijana wa Chadema kutaka kuvamia kituo yamekanushwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Malinyi, Novatus Melkiory ambaye amesema hakuna vijana wa Chadema waliofanya fujo.

"Watu tulionao hapa waliotoka Kilombero ni mbunge na viongozi wa chama tu," amesema.

Hakuna maoni: