Jumanne, 28 Novemba 2017

Muhimbili kupeleka Wataalam Saba Mafunzoni India


Wiki moja baada ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufanya upasuaji wa upandikizaji wa figo kwa mafanikio, imetangaza kupeleka wataalamu wake saba nchini India kujifunza upasuaji wa magonjwa ya ini ikiwemo upandikizaji wa ogani hiyo.

Akizungumza na wanahabari leo Jumanne Novemba 28,2017 mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya umma cha Muhimbili, Aminiel Aligaesha amesema wanapeleka wataalamu hao nje kwa mafunzo hayo.

"Timu hii ya wataalamu inajumuisha madaktari bingwa wanne wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, wauguzi wawili wanaosimamia mifumo ya hadubini na mhandisi wa vifaa tiba anayesimamia mitambo ya hadubini," amesema Aligaesha.

Amesema mafunzo hayo yatachukua miezi mitatu. Wataalamu hao wanatarajiwa kurejea nchini wiki ya kwanza ya Machi, 2018.

Aligaesha amesema wanatarajia watakaporudi wataongeza ufanisi katika uchunguzi na tiba ya magonjwa ya ini kwa kutoa mawe, kuzibua mifereji ya nyongo na kongosho iliyozibwa na uvimbe.

"Tutaweza kufanya upasuaji wa ini kuondoa uvimbe mkubwa unaodhofisha afya na kutishia maisha ya wagonjwa,” amesema.

Amesema lengo ni kujenga uwezo wa ndani kwa muda mfupi utakaowezesha kufanyika kwa upandikizaji wa ini kwa wagonjwa wenye mahitaji.

Mkuu wa kitengo cha magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, Dk John Rwegasha amesema kuna ongezeko la wagonjwa wenye matatizo ya ini hivyo ni muda muafaka kwa nchi kujikita katika matibabu hayo.

Novemba 21, mwaka huu, Muhimbili ilifanya upasuaji wa kupandikiza figo kwa mgonjwa kwa mafanikio.

Juni mwaka huu, Muhimbili ilifanya upasuaji wa kuwawekea vifaa vya kusaidia kusikia watoto watano ambao walizaliwa wakiwa hawasikii.

Hakuna maoni: