MBUNGE WA MSALALA, EZEKIEL MAIGE (CCM), AKIWA NA WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA KATIKA VIWANJA VYA BUNGENI.
Maige ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika serikali ya awamu iliyopita, alitoa ombi hilo bungeni mjini hapa jana alipokuwa anauliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mikoa (Tamisemi) kuhusu ujenzi wa zahanati na vituo vya afya jimboni kwake.
Alisema amefurahia kusikia Tanzania itapewa na Acacia Sh. bilioni 700 kwa kuwa kwa muda mrefu amekuwa akipiga kelele juu ya Watanzania, hasa wananchi wa jimbo lake, kutonufaika na rasilimali zilizopo nchini.
Maige alisema ikiwa serikali itampatie kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya jimbo lake, anaamini mradi wa ujenzi wa vituo vya afya na zahanati zaidi ya 20 unaoendelea Msalala utakamilika haraka.
Akijibu ombi hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Josephat Kandege, alisema: "Kimsingi ni wazo jema ambalo linaweza likafikiriwa".
Awali katika swali la msingi, Maige alitaka kujua serikali imejipangaje kukamilisha maboma 28 ya zahanati kwenye vijiji mbalimbali vya jimbo la Msalala.
Katika jibu lake, Kandege alisema serikali katika mwaka huu wa fedha imetenga Sh. milioni 336.742 za rukuzu ya maendeleo (CDG) kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati katika vijiji saba vya Nyamigege, Gula, Ikinda, Kalole, Jomu, Buchambaga na Ndala kati ya 31 zilizopo kwenye mpango wa ujenzi.
Alisema kuwa serikali mwaka uliopita wa fedha ilitumia Sh. milioni 277 kukamilisha ujenzi wa zahanati mpya nne ambazo zipo jimboni humo.
Alisema kuwa kati ya maboma 31 yaliyojengwa jimboni humo, matatu ni ya vituo vya afya tarajiwa ambavyo ni Isaka, Mega na Ngaya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni