BAADA ya kuhakikisha inabanana na Simba kileleni mwa Ligi Kuu Bara, klabu ya Azam FC, imesema msimu huu imedhamiria kutwaa ubingwa huo unaoshikiliwa na Yanga.
Simba ina pointi 19 kileleni sawa na Azam, lakini Wekundu wa Msimbazi hao wanaongoza msimamo huo wa ligi kutokana na kuwa na tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Wanalambalamba hao.
Akieleza kinachowapa matumaini ya kutwaa ubingwa huo, Meneja wa Azam FC, Philipo Alando, alisema wanajivunia mwenendo wao katika Ligi Kuu, wakiwa hawajapoteza mechi hata moja kama ilivyo kwa Simba, Yanga na Mtibwa Sugar.
“Wito wangu kwa mashabiki wa Azam FC ni kwamba msimu huu watarajie jambo lolote linaweza kutokea kwa sababu tumeonyesha mwanga wa tunapoelekea,”Alando ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo.
Aidha, aliwataka mashabiki hao kuendelea kuwaunga mkono wachezaji wapya chipukizi waliosajiliwa na kupandishwa kikosi cha kwanza msimu huu.
“Tunaomba watuvumilie na kuwavumilia wachezaji wao vijana, kwani baadaye watafanya makubwa,” alisema.
Baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kirafiki za kimataifa, ligi hiyo raundi ya 10 itaendelea Jumamosi na Jumapili.
Azam itakuwa ugenini kuivaa Njombe Mji huku Simba ikiwa mgeni wa Tanzania Prisons Jumamosi. Jumapili Yanga itaialika Mbeya City wakati Mtibwa Sugar ikiwa mwenyeji wa 'ndugu zao' Wakata Miwa wa Kagera, Kagera Sugar.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni