Jumatano, 8 Novemba 2017

Mbunge ajia juu taasisi ya maadili

Dodoma. Mbunge wa Ulanga (CCM) Goodluck Mlingwa amehoji majukumu ya taasisi za Serikali katika kusimamia maadili ambayo yanaporomoka kutumia matumizi ya mitandao.

Akiomba mwongozo huo bungeni leo Novemba 8, Mlingwa amesema  Taifa limeingia katika tatizo la uvunjivu wa Sheria na Katiba ya nchi ambao husababishwa na mwenendo mbovu kupita kiasi wa matumizi ya mitandao ya jamii.

“Kwa mfano mtandao wa instagram umekuwa kitovu kikubwa cha watu kujitangaza kwenye biashara za ngono, kitovu kikubwa cha mapenzi ya jinsia moja, habari za uzushi,” amesema.

Ametoa mfano wa viongozi kutoa habari za uzushi ambapo kuna mtu aliwahi kujiuzulu akaandika ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram kuwa amemuandikia barua Spika kuhusu uamuzi wake.

“Instagram imekuwa kitovu kikubwa cha kutoa taarifa za uongo, kutoa taarifa ambazo zinasababisha taharuki kwa nchi, Serikali imekuwa ikichambwa hadi kuvuliwa nguo,”amesema.

Amesema pia whatsapp kumekuwa na makundi ambayo lengo lake kubwa ni kutangaza biashara za mapenzi na kurusha picha za utupu pamoja na mambo mengine ambayo yanaharibu maadili ya nchi.

“Sasa TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Nchini) pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Utamaduni na Michezo ni lipi  jukumu lao katika hili ? Maana maadili katika Taifa letu yameporomoka. Sasa hivi wanafunzi hawa ukiwaona ni wakubwa kuliko mimi,” amesema.

Akijibu kwa upande wa Serikali, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema Serikali imesikia mbunge huyo na wanazo taarifa na kuna baadhi ya maswali ya wabunge ambayo yataulizwa katika mkutano huo wa tisa yanayofanana na jambo hilo.

“Kwa nafasi mbalimbali Serikali itaendelea kutoa ufafanuzi maelekezo ya kisheria. Hivyo tutaendelea kuboresha maadili mema katika nchi yetu kwa kupitia sheria tulizonazo kwa kadri teknolojia inayozidi kukuwa katika nchi yetu,” amesema

Mwananchi:

Hakuna maoni: