Alhamisi, 9 Novemba 2017

Mbeya: Wafanyabiashara 7 wa soko la SIDO walipwa fidia ya mali zao.

Wafanyabiashara saba tu kati ya wafanyabiashara zaidi ya 2500 ndio ambao wamelipwa fidia ya mali zao ambazo ziliteketea kwa moto wakati soko la SIDO la jijini Mbeya lilipoungua na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni 14 mwezi Agosti mwaka huu,kufuatia wafanyabiashara hao kukatia bima biashara zao.

Wafanyabiashara saba wa soko la sido jijini Mbeya ambao walikata bima ya biashara zao katika benki ya biashara ya akiba,ACB,wameonja ladha nzuri ya uamuzi wao baada ya benki hiyo kutekeleza jukumu lake la kuwalipa fidia ya mali zao inayofikia shilingi milioni 60.

Meneja wa Benki ya biashara ya Akiba,ACB,Francis Kaaya amesema mbali na kulipa fidia hiyo pia wamekuwa wakiwatembelea wafanyabiashara hao ambao ni wateja wao kwa lengo la kuwapatia elimu ili kuhakikisha wanarejesha biashara zao kama zilivyokuwa awali kabla ya kupatwa na janga la moto.

Akikabidhi hundi ya malipo ya fidia kwa wafanyabiashara hao,Mkuu wa wilaya ya Mbeya,William Paul Ntinika ametaka elimu ya umuhimu wa kukata bima itolewe kwa wafanyabiashara wote ili wazikatie bima biashara zao kama sehemu ya kujikinga na majanga mbalimbali ikiwemo moto.

Hakuna maoni: