Jumapili, 26 Novemba 2017

JKCI YAFANYA UPASUAJI WA MOYO BILA KUFUNGUA KIFUA


Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto ya nchini Israel, wamefanya upasuaji wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa watoto 20 wenye matatizo ya moyo.

Upasuaji huo ambao unatumia mtambo wa Cathlab, ulifanyika katika kambi maalumu ya matibabu iliyoanza Novemba 23 na kumalizika leo. Matibabu yaliyofanyika ni kuziba matundu na kutanua mishipa kwenye moyo.

Taarifa kutoka Kitengo cha Uhusiano na Masoko cha JKCI, ilisema katika kambi hiyo watoto 100 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi.

Taarifa hiyo ilisema watoto 60 ambao watakuwa na matatizo, watapelekwa nchini Israel kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua mwakani na watoto 40 watatibiwa nchini.

“Tumepanga kufanya matibabu kwa watoto 25, tunaamini hadi kambi itakapomalizika watoto wote hawa watakuwa wamepata matibabu,” inafafanua taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watoto 20 waliopata matibabu, tayari wengine wameruhusiwa na waliobaki hali zao zinaendelea vizuri wataruhusiwa afya zao zitakapoimarika.

Tangu mwaka 2015, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilianza kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto na hadi sasa watoto 40 wamefanyiwa upasuaji wa moyo nchini Israel.

Wakati kambi hii inaendelea, baadhi ya wafanyakazi wa JKCI walikwenda mkoani Kagera kufuatilia maendeleo ya mtoto Julius Kaijage (12) mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Green Acres iliyoko Bunazi ambaye alifanyiwa upasuaji wa moyo nchini Israel mwaka 2013.

“Tumekuwa na tabia ya kufuatilia maendeleo ya watoto tunaowafanyia upasuaji, hii inatusaidia kufahamu wanavyoendelea,” inasema taarifa hiyo na kuongeza:

“Tunatarajia kuwa na kambi nyingine ya matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima itakayoanza leo hadi Desemba mosi. Katika kambi hii ambayo tutashirikiana na wenzetu kutoka Taasisi ya Open Heart International ya nchini Australia, tunatarajia kufanya upasuaji wa kufungua kifua kwa watoto 13 na watu wazima 10.”



Hakuna maoni: