Jumatano, 8 Novemba 2017

Afungwa jela maisha kwa kumbaka mtoto

MAHAKAMA ya Wilaya ya  Mpanda  mkoani Katavi,  imemhukumu Lazaro Ngomalala (50), mkazi wa  Kijiji cha Sibwesa  wilaya ya Tanganyika kifungo cha maisha baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Chiganga Ntengwa, alisema mahakama imeridhika na ushahidi wa  mashahidi  sita wa upande wa mashtaka  uliotolewa mahakamani hapo, ukiwamo wa mwanafunzi aliyebakwa.

Kabla ya kutoa hukumu, Ntengwa  alisema mtu  yeyote  anayefanya kitendo kama alichofanyiwa  mtoto huyo,  anakuwa  amefanya kosa kwa mujibu wa kifungu cha sheria   namba 130 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili na  kifungu cha  sheria namba 131,  kifungu kidogo cha  tatu cha  kanuni ya adhabu.

Alieleza kutokana na ushahidi uliotolewa , ukiwamo wa  mtoto mwenyewe aliyebakwa na mwenzake  ambaye  alishuhudia   tukio  hilo,  mahakama pasipo  kuacha shaka  yoyote, imemkuta na hatia mshtakiwa Ngomalala.

Hakimu Ntengwa  alisema  miongoni mwa ushahidi uliosababisha mahakama imtie  mshustumiwa hatiani ni ule  uliotolewa na mtoto aliyebakwa na mwenzake mwenye umri wa miaka saba , alisema  licha ya kuwa na umri mdogo, watoto hao walitoa ushahidi  kwa ufasaha  mkubwa dhidi ya tukio hilo.

Pia  alisema mahakama  ilijiridhisha na  ushahidi uliotolewa  na   muuguzi wa  zahanati ya Sibwesa,  aliyemfanyia  uchunguzi  na kubaini  mtoto  huyo  alikuwa  amebakwa,  hali iliyomlazimu  amwanzishie  dawa ya kuzuia  maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Kabla ya  kusoma  hukumu, Hakimu alitoa  nafasi  kwa  mtuhumiwa kama  ana sababu ya msingi ya kujitetea ili aishawishi  mahakama  impunguzie  adhabu.

Katika kujitetea kwake, aliiomba  mahakama  imwachie  huru kwa kile  alichodai  kuwa  yeye  hakutenda kosa  hilo  bali   amesingiziwa na  mama  mzazi wa mtoto huyo kwa kuwa  alikuwa akimdai fedha  alizomkopesha.

Hata hivyo, Hakimu Ntengwa  alisema kutokana   na mshitakiwa  kupatikana  na  hatia, mahakama inamhukumu mshtakiwa kifungo cha maisha jela.

Awali, Wakili wa  Serikali  Fravian  Shiyo,  alidai  mahakamani  hapo kuwa   Lazaro alitenda kosa  hilo Oktoba  12,  mwaka  jana,  majira ya saa nne asubuhi kijijini hapo.

 Ilidaiwa kuwa  siku ya  tukio  mshitakiwa  alimkuta  mtoto aliyemtendea  kitendo  hicho  akiwa na mtoto  mwenzake wakiwa wanacheza  jirani na  nyumba yao ndipo  alipowadanganya wamfuate  nyumbani kwake  ili akawape fedha wakanunue biskuti na soda.

 Shiyo  alidai kuwa  wakati wakiwa wanakwenda  nyumbani kwa   mshitakiwa,  walipofika  kwenye eneo la  tangi la  maji,  Lazaro  alianza  kumbaka  na mtoto huyo kuanza kupiga  kelele,  lakini  hakumwachia  mpaka  alipo maliza  aja  yake.

Hakuna maoni: