Alhamisi, 9 Novemba 2017

ACT Wazalendo leo imetoa mambo makubwa manne

Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza mambo manne kuhusu kupekuliwa kwa  Ofisi za chama hicho na Jeshi la Polisi. Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi, Ado Shaibu imeeleza mambo hayo kuwa ni;

1. Leo Oktoba 9, 2017, Kaimu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Dorothy Semu aliitikia wito wa jeshi la Polisi (Kituo cha Makosa ya Kifedha, Kamata, Dar es salaam) waliomtaka kwenda kutoa maelezo ya ziada kuhusu nyaraka na vifaa vya kieletroniki vilivyochukuliwa kwenye Ofisi za Makao Makuu ya ACT Wazalendo

2. Ikumbukwe kuwa juzi tarehe 7 Novemba 2017 Jeshi la Polisi lilifanya upekuzi katika Makao Makuu ya ACT Wazalendo yaliyopo Kijitonyama Jijini Dar es salaam na kuondoka na nyaraka za chama kuhusu Kusinyaa kwa uchumi wa nchi na vifaa vya kielektroniki (flash na laptop) vilivyotumika kuandaa taarifa hizo za kiuchambuzi.

3. Ni zaidi ya wiki sasa tangu Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Kabwe aitwe na Jeshi la Polisi kwanza kwa tuhuma za uchochezi kisha uchambuzi wa Kamati Kuu kuhusu Kusinyaa kwa uchumi. Tangu kuitwa kwake kwa mara ya kwanza tarehe 31 Oktoba 2017 katika siku zilizofuatia yeye mwenyewe na viongozi wengine kadhaa wa Chama wameitwa kuhojiwa na Jeshi la Polisi.

4. Kama tulivyoeleza huko awali, danadana hizi za Jeshi la polisi zimeathiri kwa sehemu kubwa ushiriki wetu kwenye Kampeni za marudio ya uchaguzi wa madiwani. Hivyo basi, kuanzia sasa, viongozi wetu watatawanyika mikoani kuendelea na kampeni.

Kama jeshi la polisi litataka kuwahoji viongozi wetu litapaswa kutengeneza utaratibu ambao hauathiri ushiriki wetu wa Kampeni.

Kwa kuanzia, Kaimu Mwenyekiti wa Chama Ndugu Yeremia Kulwa Maganja atafanya ziara kwenye mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kushiriki ufunguzi wa Kampeni kwenye kata zilizopo kwenye mikoa hiyo ambazo zinarudia uchaguzi.

Hakuna maoni: